Na Mwamvua Mwinyi, Mafia

WANANCHI wa Wilaya ya Mafia mkoani Pwani wameanza kunufaika na huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili, iliyowafikia wananchi wa vijijini kwa lengo la kuwasaidia kutambua haki zao na kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria.

Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi wa Mafia ni migogoro ya ardhi, ikiwemo migogoro ya mipaka kati ya mtu na mtu, mtu na taasisi, pamoja na uvamizi wa maeneo ya wawekezaji. Changamoto hizo zimeelezwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa elimu ya masuala ya kisheria.

Kampeni hiyo iliyoanza Oktoba 29, 2026, inatekelezwa katika Halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, ambapo wananchi wanapata elimu ya sheria pamoja na fursa ya kuwasilisha changamoto zao kwa timu ya watoa huduma.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Lazaro Mushi, amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kisheria na kuwawezesha kutambua haki zao na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Amesema katika utekelezaji wa kampeni hiyo wamepokea kero mbalimbali za wananchi zinazohusu masuala ya kisheria, huku akieleza kuwa mwitikio ni mzuri na kuwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi ili huduma hizo ziwanufaishe wengi zaidi.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Michael Njenda, amesema kampeni hiyo pia inatoa elimu kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia kuanzia kwa watoto hadi watu wazima, kwa lengo la kujenga jamii inayozingatia haki na usalama wa kila mmoja.

Wananchi wa Kata ya Kanga wameishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma hizo katika maeneo yao, wakieleza kuwa hatua hiyo imewawezesha kupata elimu ya kisheria kuhusu masuala yaliyokuwa yakiwatatiza.

Zubeda Juma, mkazi wa Kijiji cha Bweni, amesema huduma hiyo imekuwa msaada kwa wananchi wa maeneo ya vijijini ambao awali walikuwa wakisikia kuhusu huduma hizo kupitia vyombo vya habari, lakini sasa wamepata fursa ya kunufaika nazo.

Kampeni hiyo inatarajiwa kutekelezwa kwa siku 10 kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 7, 2026, ambapo kata nane na vijiji 23 vya Wilaya ya Mafia vinatarajiwa kufikiwa.

Katika siku ya pili ya kampeni hiyo, huduma za msaada wa kisheria zilitolewa katika Kata ya Baleni, kupitia vijiji vya Baleni, Kungwi, Kibada na Kifinge, ambako wananchi walipata elimu ya sheria na kuwasilisha changamoto zao kwa timu ya watoa huduma