RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati alipozundua mji wa serikali Mtumba mkoani Dodoma Oktoba 30, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço ambaye ameshiriki pia akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi iliyofanyika katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma Oktoba 30, 2026
……………..
Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Katibu Mkuu Kiongozi kwa kushirikiana na makatibu wakuu kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya misitu katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, yanapandwa miti na kutunzwa ili mji huo uwe na mandhari ya kijani na kuvutia.
Ametoa maagizo hayo , Oktoba 30, 2026, wakati akiwahitubia wananchi na watumishi wa serikali baada ya kuzindua majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, huku akiwashukuru wote waliohusika na utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.
Aidha, amewataka Viongozi na watumishi wa umma kuhakikisha majengo, miundombinu, mazingira na usafi wa Mji wa Serikali Mtumba vinatunzwa vizuri ili mji huo uendelee kuwa na mandhari nzuri na yenye kuvutia.
Amesema kuwa katika ramani ya eneo la Mji wa Serikali kuna maeneo yaliyotengwa kuwa maeneo ya kijani na kuotesha misitu ambayo pia yanagawa baina ya wizara na wizara, hivyo maeneo hayo yanapaswa kutunzwa na kuwa kijani kweli. “Kama kuna mvua au kuna jua lakini misitu ile iliyokusudiwa ipandwe na ionekane Dodoma iko kijani,” amesema
Aidha, ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na mamlaka nyingine za Serikali, kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma wa mwaka 2019–2039 ili kuepuka ujenzi holela usiozingatia taratibu za mipango miji.
Pia amebainisha kuwa usimamizi huo unapaswa kuzuia shughuli zisizoendana na matumizi yaliyopangwa ya ardhi na kulinda maeneo ya huduma za jamii, hifadhi za barabara na maeneo ya wazi dhidi ya uvamizi, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma.
Pia amezitaka wizara zinazohusika na huduma za jamii kuhakikisha Mkoa wa Dodoma unapata huduma za umeme, maji na barabara kwa ukamilifu, akisema kuwa Dodoma ndio mkoa wa makao makuu ya nchi.
Aidha, ameongeza kuwa uendelezaji wa Jiji la Dodoma unahitaji ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, hivyo ameielekeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na sekta nyingine kuendelea kuhamasisha na kuweka mikakati madhubuti ya kuvutia wawekezaji kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza jiji hilo.

