Jumla ya wafanyakazi 92 wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza wakati wa mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere uliopo Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa upimaji huo dakatri bingwa wa magonjwa yatakanayo na kazi Elias Birago alisema jitahida za serikali kuwafikishia wananchi huduma za uchunguzi na matibabu katika maeneo wanayofanyia shughuli zao zimekuwa na mafanikio makubwa.

“Kambi ya uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa COPRA imewasaidia wafanyakazi hao kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua mapema ili kujikinga na madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Birago.

Aidha Dkt. Birago ameziomba taasisi, mamlaka, mashirika, na kampuni mbalimbali kuiga mfano wa COPRA wa kuhakikisha kuwa wafanyakazi wake wanapata elimu ya afya na huduma za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza pamoja na umuhimu wa kushiriki katika kampeni ya jua namba zako kwani imekuwa ikisaidia wananchi kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia ushauri wa kitalaamu kutoka kwa madaktari bingwa.

“Katika kambi hii tumetoa pia elimu kuhusu homa ya ini, ugonjwa ambao daliili zake ni ngumu kutambulika lakini pia tukawaomba wafanyakazi hawa kufika katika Taasisi yetu na matawi yake ili waweze kufanyiwa uchunguzi na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo”, alisema Dkt. Birago.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Marry Majule aliishukuru JKCI Hospital ya Dar Group kwa kuwa tayari kuwapatia elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na kuwafanyia uchunguzi wa afya.

“Ulaji wetu umekuwa si mzuri kutokana na namna tunavyoishi hivyo kupitia huduma hii ya JKCI Hospitali ya Dar Group tumepata elimu itakayotusaidia kuchukua hatua za kulinda afya zetu na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwani afya bora inatusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi katika kuwahudumia wakulima na wadau wote wa nafaka na mazao mchanganyiko”, alisema Marry.