Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali mkoani Mwanza, kwa lengo la kuongeza uelewa wao kuhusu mchakato huo na kuwaandaa kushiriki katika hatua za kutoa maoni.
Zoezi hilo lililofanyika leo, Oktoba 29, 2026, na kuzinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP Salum Rashid Hamduni, limehusisha viongozi wa Serikali ya Mkoa na wilaya, wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, taasisi za dini, mashirika ya kiraia, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Ushirikishwaji wa makundi hayo unalenga kuwapatia taarifa na uelewa kuhusu maudhui ya rasimu hiyo, umuhimu wa Fungamano la Kisiasa la EAC na hatua zinazohusika katika mchakato wake. Aidha, zoezi hilo linawaandaa wadau kutoa maoni na mapendekezo yao wakati wa mchakato rasmi wa ukusanyaji maoni utakapoanza.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Tanzania kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa kuelekea Fungamano la Kisiasa la EAC, kwa kuzingatia umuhimu wa uelewa wa umma na mchango wa wadau katika kujenga mustakabali wa ushirikiano wa kikanda.
Ujumbe wa Wizara katika zoezi hilo uliongozwa na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bi. Mwanamridu Amiry Jumaa.

