Na, Mwandishi wetu – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Prof. Palamagamba Kabudi amekagua na kuridhishwa na maandalizi ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, leo tarehe 29 Oktoba, 2026.
Akiwa katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo amekagua maeneo mbalimbali yatakayotumika katika hafla ya uzinduzi, yakiwemo geti kuu la kuingilia Mji wa Serikali, eneo la uwekaji jiwe la msingi la uzinduzi wa barabara za lami, eneo la uwekaji jiwe la msingi la uzinduzi wa majengo ya Serikali, pamoja na Uwanja wa Mashujaa utakaotumika kufanyika kwa hafla hiyo.
Profesa Mkumbo amepongeza hatua ya maandalizi iliyofikiwa na kutoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia tukio hilo la kihistoria katika Taifa letu.
Katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo aliambatana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi; Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. James Kilabuko; Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, Bw. Paul Sangawe, pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika kesho, tarehe 30 Oktoba, 2026, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiambatana na Mgeni Maalum Rais wa Jamhuri ya Angola Mhe.João Manuel Gonçalves Lourenço watashuhudia hafla ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

