Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam.

MAKUNDI maalum yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu yamepata fursa za kiuchumi zenye thamani ya Shilingi bilioni 82.34 kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NEST), unaowezesha makundi hayo kushiriki katika zabuni za Serikali.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo Octooba 29,2026 jijini Dar es Salaam kwenye kikao kazi cha kilichoandaliwa na ofisi ya msajili wa hazina(ORT), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema mfumo huo umesaidia kuondoa baadhi ya vikwazo vilivyokuwa vikikabili makundi maalum katika kupata na kushiriki zabuni za umma.

Amesema kupitia mfumo huo, vijana wamepata zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 44.74, wanawake Sh bilioni 33.51, wazee Sh bilioni 3.78, huku watu wenye ulemavu wakipata Sh milioni 680.

Simba amesema hadi sasa makundi maalum 33,659 yamesajiliwa katika mfumo huo na kupata fursa za kufanya kazi mbalimbali za Serikali, ikiwemo ujenzi, usafi na utengenezaji wa madawati ya shule.

Amesema PPRA inaendelea kutoa elimu kwa makundi hayo ili kuyawezesha kuelewa taratibu za ununuzi wa umma na namna ya kutumia mfumo wa NEST kupata zabuni zinazotangazwa na taasisi za Serikali.

Akizungumzia manufaa ya mfumo huo, Mwenyekiti wa Kikundi cha Nyota Bora, Godwin Mmisi, amesema maboresho yanayofanywa na PPRA yameongeza uelewa wa makundi maalum kuhusu fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali.

Mmisi, ambaye pia ni kiongozi wa vikundi vinavyojihusisha na shughuli za ubebaji mizigo katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Ubungo, amesema awali makundi hayo yalikuwa yakikabiliwa na changamoto ya kutambua namna ya kuzifikia fursa zilizotengwa kwa ajili yao.

Amesema elimu inayotolewa na PPRA imewasaidia kuelewa taratibu za kuingia katika mifumo ya ununuzi wa umma na kupata ufafanuzi kuhusu namna ya kushiriki katika zabuni mbalimbali.

“Tunashukuru Serikali kwa kutupatia fursa hizi. PPRA imekuwa ikitusaidia kwa kutupatia elimu na ufafanuzi kuhusu namna ya kutumia mifumo hiyo ili nasi tuweze kunufaika na fursa za kiuchumi,” amesema Mmisi.

Amesema kwa sasa wanachama wa vikundi hivyo wanaendelea kufanya shughuli za kubeba mizigo katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Ubungo, na kupata kipato kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.

Kwa upande wake… .Simba amesema mfumo wa NEST umewezesha utoaji wa zabuni 403,643 zenye thamani ya Sh trilioni 42.6 na kuokoa takribani Sh bilioni 28 kupitia kupunguza matumizi ya karatasi na nyaraka mbalimbali za ununuzi.

Amesema kiwango cha uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa umma kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 79 mwaka 2025/26, akieleza kuwa hatua za udhibiti, ikiwemo kuwafungia baadhi ya kampuni zilizokiuka sheria, zimechangia kuimarisha uzingatiaji huo.

Ameongeza kuwa mfumo huo umepunguza muda na gharama za usafiri kwa wazabuni, kwa kuwa sasa wanaweza kufuatilia taarifa za zabuni na kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi husika.

Simba amesema zaidi ya benki 36 zimeunganishwa na Mfumo wa Bank Security Portal ili kurahisisha utoaji na uhakiki wa dhamana za zabuni, huku watumiaji wakihimizwa kutumia programu ya NEST Tender inayopatikana Play Store na App Store kufuatilia taarifa za zabuni na hali ya malipo.

Amesema PPRA itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa umma kwa lengo la kuimarisha uwazi, ushindani wa haki na kuongeza ushiriki wa wazawa katika zabuni za Serikali na kukuza uchumi wa taifa.