Na Sophia Kingimali.
MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuandaa mpango mkakati wa kuwawezesha vijana na kampuni za Kitanzania kushiriki katika miradi ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Amesema maandalizi ya wataalamu wazawa yanapaswa kuanza mapema kabla ya utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwamo bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) na mradi wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG), ili Watanzania wanufaike na ajira na fursa za biashara.
Ndejembi alitoa maagizo hayo leo Octoba 28,2026 Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utiaji saini leseni za utafutaji wa mafuta na gesi katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara.
Amesisitiza kuwa serikali inalenga kuhakikisha uwekezaji katika sekta hiyo hauishii kwenye utafutaji na uzalishaji pekee, bali unawawezesha Watanzania kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani kupitia ajira, huduma na usambazaji wa bidhaa.
Amesema kuchelewa kuwaandaa vijana na kampuni za ndani kutasababisha kukosa fursa zitakazojitokeza wakati miradi hiyo itakapoanza kutekelezwa, hivyo amezitaka mamlaka husika kuchukua hatua mapema.
Ndejembi ametoa mfano wa Rusiba Manjila, mtaalamu wa mafuta na gesi aliyerejea nchini kutoka Saudi Arabia na kuanzisha kampuni yake, ambayo imeajiri Watanzania zaidi ya 50, huku asilimia 80 wakitoka kijiji cha Madimba ambako mradi wa gesi unatekelezwa.
Amesema mfano huo unaonesha kuwa uwekezaji katika ujuzi na utaalamu wa wazawa unaweza kusaidia kuanzisha kampuni za Kitanzania na kuongeza ajira, hivyo ametaka vijana wanaohitimu vyuo nchini kuandaliwa kulingana na mahitaji ya sekta hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zinahitaji mtaji mkubwa, teknolojia ya kisasa na utaalamu maalumu, huku bajeti ya utafutaji ikikadiriwa kuwa kati ya dola za Marekani milioni 15 na milioni 30, ambapo takribani asilimia 70 hutumika katika shughuli za uchorongaji.
Kutokana na gharama hizo, amesisitiza umuhimu wa TPDC kushirikiana na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha na kiteknolojia, huku ikihakikisha uwekezaji unaofanyika unalinda maslahi ya taifa na kutoa nafasi kwa kampuni za ndani.
Amesema rasilimali za mafuta na gesi zina mchango muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, hivyo usimamizi wake unapaswa kuzingatia sheria, matumizi bora ya fedha, usalama na uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, amesema utiaji saini leseni hizo ni hatua muhimu katika kuongeza shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, akimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini.
Homera amesema utoaji wa leseni hizo unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, inayowezesha TPDC kutekeleza majukumu ya utafutaji na uendelezaji wa rasilimali hizo kwa kuzingatia sheria na maslahi ya taifa.
Amesema hadi Septemba 2026, Tanzania ilikuwa na vituo 22 vya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG), karakana 20 za kufunga mifumo ya gesi kwenye magari, magari 2,020 yanayotumia gesi hiyo, viwanda 57, taasisi 31 na kaya takribani 3,000 zilizounganishwa na bomba la gesi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati na TPDC kusimamia utekelezaji wa leseni hizo, huku akisisitiza umuhimu wa ajira, mafunzo na kuwaendeleza wataalamu wazawa ili rasilimali hizo zichangie maendeleo ya taifa.


