Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema kuwa uzinduzi wa miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza Oktoba 27, 2026 jijini Dodoma na waandishi wa habari, Kuelekea uzinduzi wa miundombinu hiyo utakaofanyika Oktoba 30, 2026 katika Mji wa Serikali Mtumba, huku mgeni rasmi anatarajiwa Kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. huki akiwataka wananchi, hususan wa Mkoa wa Dodoma, kujitokeza kwa wingi kushuhudia hafla hiyo, ambayo itatanguliwa na upigaji wa fataki usiku wa kuamkia Oktoba 30.
Aidha, amesema kuwa hafla hiyo itahusisha uzinduzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za serikali pamoja na barabara za kiwango cha lami katika Mji wa Serikali Mtumba, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu yenye miundombinu bora na mazingira rafiki ya kufanyia kazi.
Amesema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi ilianza Novemba 28, 2018 na ilihusisha ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za muda pamoja na majengo ya Wakala Mkuu wa Serikali na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ambapo jumla ya Sh bilioni 39.39 zilitumika.
Aidha, amebainisha kuwa awamu ya pili ilianza Oktoba 2021 na inahusisha ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya huduma za kijamii pamoja na majengo ya wizara na taasisi, ambapo jumla ya majengo 37 yamejengwa, kati yake 24 ni ya wizara na 13 ni ya taasisi, huku gharama za makadirio ya ujenzi zikiwa Sh bilioni 940,085,598,230.17.
Ameongeza kuwa katika Mji wa Serikali Mtumba zimejengwa barabara zenye jumla ya kilomita 57.1 ambazo zote zimewekwa lami pamoja na taa, huku ujenzi wake ukigharimu Sh bilioni 110.5. Amesema uwepo wa wizara na taasisi katika eneo moja utarahisisha uratibu wa shughuli za serikali, mawasiliano baina ya taasisi na utoaji wa huduma, sambamba na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali.
Prof. Kabudi amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi na wafanyabiashara kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya Mji wa Serikali na Dodoma kwa ujumla, akibainisha kuwa kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kutasaidia kuongeza idadi ya watu wanaofika Dodoma na hivyo kuongeza fursa za kiuchumi.
Aidha, amewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali kutumia vizuri miundombinu hiyo na kuhakikisha mazingira hayo yanaimarisha uwajibikaji, uadilifu, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, akisisitiza kuwa majengo mazuri pekee hayatoshi bila utendaji bora na nidhamu ya kazi.

