Na Sophia Kingimali

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Richard Muyungi, amezitaka nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za ziwa hilo ili kukabiliana na upungufu wa samaki unaotishia maisha na shughuli za kiuchumi za mamilioni ya wananchi.

Akizungumza leo Oktoba 25, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Kamati ya Usimamizi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Muyungi amesema maamuzi ya mkutano huo yanapaswa kutafsiriwa katika hatua zinazotekelezeka kwa ajili ya kulinda ziwa hilo.

Amesema Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu kiikolojia na kiuchumi, inayotegemewa na zaidi ya watu milioni 13 katika nchi nne kupitia shughuli za uvuvi, usafirishaji, uhifadhi wa viumbehai na upatikanaji wa chakula.

Ametaja changamoto zinazolikabili ziwa hilo kuwa ni mabadiliko ya tabianchi, uvuvi usio endelevu na uchafuzi wa mazingira, akizitaka nchi wanachama kutekeleza maamuzi ya mikutano na kulipa michango ya kifedha kwa wakati.

Aidha, amezihimiza nchi wanachama na sekretarieti ya mamlaka hiyo kuandaa miradi inayoweza kupata ufadhili kutoka mifuko ya kimataifa, ikiwemo Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (Global Environment Facility).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Dkt. Emma Teresa Liwenga, amesema tafiti za hivi karibuni zimeonesha upungufu mkubwa wa samaki, hali inayohitaji hatua za kudhibiti uvuvi haramu na kuboresha usimamizi wa shughuli za uvuvi.

Amesema ziwa hilo lina fursa nyingi za kiuchumi kupitia uvuvi, utalii na usafirishaji, hivyo ni muhimu kuhakikisha rasilimali zake zinasimamiwa kwa uendelevu ili ziendelee kunufaisha jamii zinazozunguka bonde hilo.

Dkt. Liwenga amesema uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi vinaathiri mifumo ya ikolojia, huku ongezeko la kina cha maji likisababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo na upanuzi wa miji kandokando ya ziwa ukiongeza changamoto ya uchafuzi.

Amesema mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya nchi zinazozunguka ziwa katika uhifadhi wa mazingira na bayoanuwai kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Mfumu Richard, amesema ziwa hilo ni muhimu kwa nchi wanachama kutokana na mchango wake katika upatikanaji wa maji, uvuvi, bayoanuwai na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Amesema pamoja na umuhimu huo, ziwa linakabiliwa na changamoto za uvuvi usio endelevu, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa makazi ya viumbehai, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu.

Richard amesema mkutano huo unajadili nyaraka na ripoti mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa shughuli za mamlaka, ikiwemo ripoti ya mwaka ya LTA pamoja na mpango kazi na bajeti ya mwaka 2027.

Amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza rasilimali za kifedha kwa ajili ya usimamizi na ulinzi wa ziwa hilo ili liendelee kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Naye Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kemilembe Mutasa, amesema Ziwa Tanganyika si mpaka wa kijiografia unaotenganisha nchi wanachama, bali ni rasilimali inayowaunganisha kupitia mchango wake katika maisha, usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.