Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amezitaka taasisi za sekta ya uchukuzi kuweka mkakati wa kusafirisha makasha 1,000 ya mizigo kila siku kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoani na nchi jirani kwa kutumia reli, ili kupunguza msongamano bandarini na barabarani.
Profesa Mbarawa alitoa maagizo hayo jana alipotembelea Kituo cha Bahi mkoani Dodoma, kinachotumika kuhamisha makasha kutoka reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kwenda reli ya zamani ya Meter Gauge Railway (MGR).
Alisema zaidi ya makasha 3,000 hushushwa bandarini kila siku na idadi hiyo inaendelea kuongezeka, hivyo kuna haja ya kuimarisha usafirishaji wa mizigo kwa reli.
Aliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Usafiri wa Majini Tanzania (TASAC) kushirikiana kuboresha upokeaji wa mizigo katika vituo vya Bahi na Isaka mkoani Shinyanga.
Alisisitiza umuhimu wa kuboresha nyaraka za usafirishaji ili makasha yanayopelekwa maeneo ya ndani ya nchi na nchi jirani yaoneshe Bahi au Isaka kama vituo vya mwisho vya kupokelea mizigo.
Alisema hatua hiyo itawawezesha wafanyabiashara kupokea mizigo yao katika vituo husika badala ya kulazimika kufuata makasha Dar es Salaam, huku ikipunguza malori yanayoingia bandarini na msongamano barabarani.
Aidha, aliwataka viongozi wa taasisi hizo kujifunza kutoka Misri kuhusu mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda maeneo ya ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Shiwa, alisema safari ya makasha kutoka Dar es Salaam hadi Bahi kwa SGR huchukua takribani saa tano, huku mizigo inayosafirishwa hadi Isaka ikiweza kufika ndani ya saa 24.
Alisema TRC itaendelea kutumia miundombinu ya reli iliyokamilika kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo nchini.

