Na WMJJ, Dar Es Salaam
Wamiliki na Walezi wa vituo vya Kulelea watoto wadogo mchana wameanza mafunzo ya siku 6 yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kutoa huduma katika vituo vyao pamoja na kupitia mwongozo uitwao Kiongozi cha Mlezi kama nyenzo muhimu ya kutimiza manukumu yao.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Eliakim Maswi akizungumza kwa niaba ya Waziri Dkt.Dorothy Gwajima wakati akifungua Mafunzo hayo, Oktoba 23, 2026, amewataka kuhakikisha, uanzishwaji na usajili wa vituo hivyo unazingatia Sheria ya Mtoto Sura ya 13 na kanuni zake.
Maswi ameelekeza, kuhakikisha Kiongozi hicho cha Mlezi kitakapokamilika kila kituo cha kulelea watoto wadogo mchana kutumia nyenzo hii katka ujifunzaj wa watoto na si vinginevyo.
“Wadau wote wa huduma za malezi mlioko hapa na ambao hawajafika mshirikiane na Serikali kuhakikisha nyenzo hii inawafikia walaji na kuwajengea uwezo ili waweze kuitumia kwa manufaa ya watoto wetu. Hivyo naelekeza jambo hili mliweke kwenye Mipango yenu endelevu. amesisitiza Maswi.
Aidha, amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha wanasimamia huduma zinazotolewa katika vituo hivyo, ikiwa ni pamoja na Malezi, Usalama na Umahiri wa Ujifunzaji wa Mapema, kuhakikisha kuwa watoa huduma (Walezi) wanajengewa uwezo wa kutoa huduma za Malezi na ujifunzaji wa mapema kwa watoto pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kubani wadau watakaosaida kusambaza kiongozi hiki kikamilifu.
Amesisitiza pia kwamba, Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana kutoa huduma kwa watoto wa chini ya miaka mitano na wanapofikisha miaka mitano na kuendelea wakahudumiwe na Wizara ya Elimu kupitia madarasa ya awali na kuendelea na si vinginevyo.
Maswi ameongeza kuwa, huduma za malezi ya watoto Wadogo (ECD) ni ajenda muhimu kwa maendeleo ya taifa na kupitia juhudi za Serikali na Washirika wa Maendeleo, inawezekana kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata huduma bora za malezi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Amina Mfaki, amesema TAMISEMI inatambua umuhimu wa mafunzo hayo katika kuimarisha malezi kwenye ngazi zote za ukuaji na utendaji wa kila siku wa malezi, vilevile inahakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia ukuaji bora wa watoto.
Naye Mkurigenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi na Makuzi nchini TECDEN, Mwajuma Kibwana
amesema wadau wanafarijika kuona Serikali ilivyojipanga kutekeleza Dira 2050 huku Kiongozi cha mlezi pamoja na mafunzo haya yakiwa ni uwekezaji unaokwenda kujenga msingi wa rasilimali watu kufikia Dira 2050.
“Vituo hivi ni mlango wa ulinzi na usalama wa mtoto, pia ni mlango wa kupata lishe nzuri.TECDEN na UVIWATA tuko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali.” amesema Mwajuma.

