Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetula, amewataka wataalam wa ununuzi na ugavi nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma, uadilifu, uwazi na uwajibikaji ili kuhakikisha Serikali inapata thamani halisi ya fedha katika matumizi ya rasilimali za umma.

Amesema rushwa, udanganyifu, mgongano wa maslahi na matumizi mabaya ya mali za umma ni vitendo vinavyopaswa kukemewa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa wataalam hao wana wajibu wa kulinda rasilimali za taifa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Luswetula ameyasema hayo Oktoba 23, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 15 ya Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), yaliyofanyika katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar.

Amesema utekelezaji wa majukumu ya ununuzi na ugavi unahitaji wataalam wenye ujuzi, weledi na uadilifu, ambao watazingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, pamoja na taratibu na miongozo iliyowekwa ili kuimarisha ushindani, kudhibiti gharama na kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 583 wametunukiwa vyeti vya kitaaluma, ambapo 453 wamehitimu Shahada ya Juu ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi (Certified Procurement and Supply Professional – CPSP-T), 64 wamehitimu Stashahada ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi (Professional Diploma in Procurement and Supply), huku 11 wakihitimu Stashahada ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi, na wengine wakikamilisha mafunzo yao katika fani hiyo.

Luswetula ameipongeza PSPTB kwa kuandaa mahafali hayo na kuendelea kuimarisha taaluma ya ununuzi na ugavi nchini, akitaja pia kuanzishwa kwa mafunzo maalumu ya ukaguzi wa mnyororo wa ugavi kuwa hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa taasisi kubaini mapungufu na kuimarisha usimamizi wa rasilimali.

Aidha, ameitaka PSPTB kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), katika kuimarisha maadili na weledi wa wataalam.

Amesisitiza kuwa taasisi na waajiri wa sekta ya umma na binafsi wanapaswa kuhakikisha nafasi za ununuzi na ugavi zinajazwa na watumishi wenye sifa stahiki, huku wakiwapa fursa za mafunzo endelevu ili kuendana na mabadiliko ya sheria, teknolojia na mahitaji ya kazi.

Ameongeza kuwa matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) yanapaswa kusaidia kuimarisha uwazi, kufuatilia utekelezaji wa mikataba na kuhakikisha shughuli za ununuzi zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Vilevile, ameitaka PSPTB kushirikiana na PPRA kufanya tathmini ya ufanisi wa mifumo ya kidijitali, ikiwemo kuunganisha Mfumo wa Usajili wa PSPTB (ORS) na mfumo wa NeST, ili kurahisisha uhakiki wa sifa za kitaaluma na kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu.

Naibu Waziri huyo amewahimiza wahitimu kuendelea kujifunza, kutumia maarifa waliyoyapata kutatua changamoto za taasisi zao na kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha mnyororo wa ugavi unasimamiwa kwa ufanisi, uwajibikaji na kuzingatia maslahi ya umma.

Amesema Serikali inatambua mchango wa wataalam wa ununuzi na ugavi katika maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu kwao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, kutunza kumbukumbu sahihi, kufuatilia mikataba na kutekeleza mapendekezo ya wakaguzi kwa wakati.

Akihitimisha hotuba yake, Luswetula amewapongeza wahitimu wote kwa hatua waliyoifikia na kuwataka kutumia vyeti vyao kama chachu ya kuimarisha utendaji katika maeneo yao ya kazi, akisisitiza kuwa mafanikio yao yatapimwa kwa mchango watakaoutoa katika kuboresha usimamizi wa ununuzi na ugavi nchini.

Mahafali hayo ya 15 ya PSPTB yamekuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha taaluma ya ununuzi na ugavi na kuongeza idadi ya wataalam wenye uwezo wa kusimamia ununuzi, mikataba, uhifadhi na usambazaji wa mali kwa kuzingatia ufanisi na thamani halisi ya fedha.