Uongozi wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Dkt. Mwamini Tulli, na Mkuu wa Chuo, Prof. Eliamani Sedoyeka, umekutana jijini Paris na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa UNESCO anayeshughulikia Elimu, Prof. Qun Chen, kujadili kuanzisha ushirikiano wa kimkakati baina ya taasisi hizo.
Prof. Sedoyeka ameeleza nafasi ya IAA katika kuandaa wataalamu wa uhasibu, fedha, biashara na TEHAMA, pamoja na dhamira ya kupanua ushirikiano wa kimataifa katika mafunzo na utafiti.
Kwa upande wake, Prof. Chen ameonesha utayari wa UNESCO kushirikiana na IAA katika kuwaendeleza walimu, utafiti na kuanzisha UNESCO Chairs kama kiungo cha ushirikiano wa kitaaluma na taasisi za nchi nyingine.
Prof. Chen aliambatana na Bw. Carlos Vargas-Tamez, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Walimu wa UNESCO, na Bi. Maya Prince, Meneja wa Programu ya UNITWIN/UNESCO Chairs.
Ziara hiyo na mazungumzo hayo vimeratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa, kwa ushiriki wa Balozi Mhe. Saidi Yakubu.

