Meneja Masoko wa Lumac Window, Renatus Tabaro akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma wanazotoa jijini Arusha .
………….
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Matumizi ya vifaa vya ujenzi vinavyounganisha uimara na mwonekano wa kisasa yameendelea kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya ujenzi, huku kampuni ya Lumac Window ikitumia maonesho ya AQRB jijini Arusha kutangaza suluhisho zake za bidhaa za Aluminium.
Kampuni hiyo imeonyesha bidhaa mbalimbali zikiwamo milango, madirisha na mifumo ya kutenganisha maeneo ndani ya majengo, ikiwa na lengo la kuwafikia wateja wanaotafuta vifaa vinavyokidhi mahitaji ya majengo ya kisasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha kuhusu ushiriki huo, Meneja Masoko wa Lumac Window, Renatus Tabaro amesema maonesho hayo ni fursa muhimu ya kujenga uhusiano na wataalamu wa ujenzi pamoja na kuwafahamisha kuhusu bidhaa zinazopatikana katika kampuni hiyo.
Tabaro amesema wameamua kushiriki ili kukutana na wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi kutoka Tanzania na nchi jirani, ambao wana nafasi muhimu katika kushauri na kusimamia matumizi ya vifaa vinavyofaa katika miradi mbalimbali ya ujenzi.
Amebainisha kuwa aluminium ina faida kadhaa katika ujenzi, ikiwamo uwezo wa kustahimili kutu na kuchangia mwonekano wa kuvutia wa majengo, jambo linaloifanya kuwa chaguo linaloweza kukidhi mahitaji ya majengo ya makazi na biashara.
Tabaro ameongeza kuwa kampuni hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha viwango vya ujenzi kwa kuhamasisha matumizi ya bidhaa zenye ubora na zinazoweza kukidhi mahitaji ya watumiaji.
“Kupitia maonesho hayo, Lumac Window inaendelea kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya ujenzi kufahamu bidhaa zake na kupata uelewa kuhusu namna milango, madirisha na mifumo ya aluminium inavyoweza kutumika katika kuboresha majengo ya kisasa.”amesema Tabaro.
