WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania inauchukulia usalama wa chakula kuwa sehemu muhimu ya usalama wa taifa na msingi wa kudumisha uthabiti wa uchumi.

Amesema upatikanaji wa chakula na lishe ya uhakika una mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi na kuiwezesha Serikali kusimamia viashiria vingine vya uchumi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumatano, Oktoba 21, 2026) wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Kituo cha Mikutano cha Iowa, jijini Des Moines, Marekani, kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue).

Waziri Mkuu ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema: “Usalama wa chakula nchini Tanzania ni suala la usalama wa taifa. Tunapokuwa na uthabiti katika upatikanaji wa chakula na lishe, tunakuwa katika nafasi salama zaidi ya kusimamia viashiria vingine vya kiuchumi.”

Dkt. Mwigulu alisema uzoefu wake katika kuongoza Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Fedha umemwezesha kuona uhusiano wa moja kwa moja kati ya uzalishaji wa chakula na uthabiti wa uchumi.

Alisema Tanzania imeendelea kuonesha ustahimilivu licha ya changamoto za kiuchumi zilizoikumba dunia hivi karibuni, hali ambayo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uthabiti wa uzalishaji wa chakula.

“Kufikia usalama wa chakula kunahitaji uwekezaji endelevu, ubunifu wa kisayansi, kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, sera madhubuti na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za utafiti,” alisema Waziri Mkuu. 

Akieleza mwelekeo wa Tanzania, alisema Serikali inalenga kubadilisha mfumo mzima wa kilimo na chakula kwa kuongeza tija, kuimarisha minyororo ya thamani, kupanua usindikaji wa mazao na kuboresha mifumo ya usafirishaji na ugavi.

Alisema hatua hizo zinalenga kuhakikisha sehemu kubwa zaidi ya thamani inayotokana na kilimo inabaki ndani ya nchi, huku wakulima wakipata fursa zaidi na vijana wakinufaika na ajira.

Akijibu swali kuhusu hatua za kuwavutia vijana kwenye kilimo, Waziri Mkuu alisema Serikali ilibaini kuwa upatikanaji wa ardhi, mitaji na mtazamo hasi kuhusu kilimo ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyowakabili. “Tumeanza kuwajengea vijana mtazamo mpya kwamba kilimo ni biashara kama biashara nyingine yoyote. Ni kazi yenye heshima na inaweza kumwezesha mtu kupata kipato kizuri na kujenga maisha bora,” alisema.

Alifafanua kuwa kupitia mpango wa Build a Better Tomorrow (BBT), Serikali inaandaa maeneo ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na kuwawezesha vijana kuingia katika uzalishaji unaozingatia fursa zilizopo katika maeneo husika.

Alisema baadhi ya vijana wanaelekezwa katika uzalishaji wa mbegu bora ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa mbegu zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewakaribisha wawekezaji kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji, akieleza kuwa nchi ina rasilimali za maji na maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo ambayo bado hayajaendelezwa kikamilifu.

Akijibu hoja kuhusu uwezekano wa kuwekeza kwenye miradi ya umwagiliaji, Waziri Mkuu alisema mipango ya miundombinu ya maji inapaswa kuzingatia pia mahitaji ya kilimo na mifugo, pamoja na matumizi ya majumbani. “Hii ina maana kwamba miundombinu ya maji haipaswi kuishia katika matumizi ya majumbani au huduma nyingine pekee, bali inapaswa kusaidia pia shughuli za uzalishaji mali, ikiwemo kilimo na ufugaji,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa. Pia, aliwahimiza wanasayansi, watafiti na wabunifu, hususan vijana, kuendeleza suluhisho zinazoongeza tija ya kilimo, usalama wa chakula na lishe.

Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, Balozi wa Tanzania Washington, Dkt. Elsie Kanza na watendaji wengine wa Serikali.