Msajili wa heshima wa Taasisi ya Wakadiriaji Gharama za Ujenzi na Miundombinu ya Uganda.(CICCQSU) QS Samuel Eric Bayo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo

Happy Lazaro, Arusha.

Arusha .Msajili wa heshima wa Taasisi ya Wakadiriaji Gharama za Ujenzi na Miundombinu ya Uganda.(CICCQSU) QS Samuel Eric Bayo, amesema Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza taaluma hiyo nchini Uganda, akieleza kuwa wataalamu wengi wa awali walipata elimu na uzoefu wao kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

QS Bayo ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa sita wa mwaka 2026 unaofanyika jijini Arusha .

QS Bayo amesema historia hiyo imejenga msingi imara wa taaluma ya ukadiriaji gharama za ujenzi nchini Uganda, huku baadhi ya wataalamu walionufaika na mafunzo hayo wakishika nafasi za uongozi katika bodi, taasisi za kitaaluma na vyuo vikuu.

Amefafanua kuwa,miongoni mwa wataalamu waliochangia kuwajengea uwezo wanataaluma wa Uganda ni QS Makoba na QS Maro, pamoja na wengine ambao walisaidia kuendeleza taaluma hiyo na kukuza kizazi cha wataalamu wenye ujuzi.

Bayo, ambaye pia ni miongoni mwa wataalamu waliosoma Tanzania kupitia mpango wa kubadilishana wanafunzi kati ya nchi hizo, amesema anaithamini nafasi ya Tanzania katika historia ya taaluma hiyo Uganda na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo.

Akizungumzia Kenya, amesema nchi hiyo nayo ilinufaika na nafasi yake ya kihistoria ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi kutoka Tanzania na Uganda, hivyo nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kuendeleza ushirikiano wa kitaaluma badala ya kuzingatia tofauti za kihistoria.

“Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda unaendelea kuimarika kupitia miradi ya pamoja, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi, hivyo wataalamu wa nchi hizo wanapaswa kubadilishana maarifa ili kuboresha sekta ya ujenzi na maendeleo ya miundombinu.”amesema QS Bayo.

Aidha, QS Bayo amesema kuwa mikutano ya kitaaluma ni fursa ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha mahusiano baina ya wataalamu wa nchi mbalimbali.

Hata hivyo QS Bayo amewataka wataalamu wa sekta ya ujenzi kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuboresha ufanisi, usahihi na kasi ya utekelezaji wa majukumu yao katika miradi ya ujenzi na miundombinu.

Amesema alipokuwa akisoma takribani miaka 22 iliyopita, wataalamu walitumia vifaa vya kuchorea kama rula maalumu na T-square, huku uchukuaji wa vipimo na ukadiriaji wa gharama ukifanyika kwa mikono kabla ya matumizi ya teknolojia za kompyuta kuongezeka.

Amefafanua kuwa matumizi ya CAD, yaani teknolojia ya kuchora michoro kwa kutumia kompyuta, yalibadilisha utendaji wa wasanifu majengo, wahandisi na wakadiriaji gharama za ujenzi, na sasa sekta hiyo inaendelea kupokea teknolojia za Akili Unde (AI) na BIM.

QS Bayo amesema BIM, inayowezesha kuunganisha taarifa mbalimbali za mradi katika mfumo wa kidijitali, imeendelea kupanuka hadi katika mifumo ya 5D inayojumuisha gharama na muda wa utekelezaji, pamoja na mifumo ya 8D inayohusisha usimamizi wa majengo na mali za mradi.

Amesisitiza kuwa wataalamu wanapaswa kujifunza na kutumia teknolojia hizo mpya ili kuongeza ushindani na ubora wa kazi zao, huku Tanzania, Uganda na Kenya zikiendelea kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kutumia teknolojia za kisasa katika kusimamia gharama, muda na ubora wa miradi ya miundombinu ya Afrika Mashariki. Washiriki mbalimbali wakiwa kwenye mkutano mkuu wa sita wa mwaka 2026 unaofanyika jijini Arusha