Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Kaster Ngonyani, amewataka wananchi kuendelea na kampeni ya “Ongea na Kamanda” katika mtaa wa Tulieni Kata ya Nsemulwa, Wilaya ya Mpanda, inayotekelezwa na Jeshi la Polisi yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za uhalifu ili kuendelea kudumisha amani, utulivu na usalama wa jamii.

Akizungumza kwenye kampeni hiyo, Oktoba 20, 2026 Kamanda Ngonyani aliwasisitiza wananchi umuhimu wa kuendelea kudumisha amani na usalama, usalimishaji wa silaha haramu, udhibiti wa uhalifu katika kutoa taarifa, wizi wa mtandaoni na kukemea vitendo vya ukatili, unyanyasaji na udhalilishaji huku akieleza umuhimu wa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kubaini, kutanzua na kudhibiti vitendo vya kihalifu.

Aidha Kamanda Ngonyani amewakumbusha wananchi kuwa jukumu la ulinzi na usalama ni la kila mmoja, hivyo amesisitiza umuhimu wa kuunda na kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi kwa kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa mali zao pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na viashiria vyake kwa wakati kwa Jeshi la Polisi kabla ya uhalifu kutendeka na kuleta madhara kwa jamii.

Vilevile, wananchi wamepata fursa ya kutoa maoni, kuuliza maswali, pongezi, ushauri na kueleza changamoto zinazowakabili katika masuala ya ulinzi na usalama huku wakieleza kufurahishwa na fursa waliyoipata ya kuwasilisha maoni na changamoto zao za kiusalama moja kwa moja kwa Kamanda wa Polisi Mkoa.