
Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) ilifanikiwa kujenga laini maalum ya umeme kutoka Gongolamboto, Dar es Salaam hadi eneo la mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), lililopo Rufiji, mkoani Pwani.
Mradi huo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ulihusisha ujenzi wa laini ya umeme wa msongo wa kilovolti 33 yenye urefu wa kilomita 245, iliyogharimu shilingi bilioni tisa.
Utekelezaji wa mradi huo uliwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kurahisisha shughuli mbalimbali za ujenzi wa mradi wa JNHPP.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 unakamilika kwa wakati, ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
ETDCO ni kampuni tanzu ya TANESCO, imeendelea kushiriki katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
