Mbunge anayewakilisha watu wenye ulemavu kutoka Rwanda ,Alex Bahati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
………….
Happy Lazaro,Arusha
Arusha. Bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA). limehimizwa kuchukua hatua za kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa kwa vitendo, kwa kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha kupata huduma na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii bila vikwazo.
Wito huo umetolewa na Mbunge anayewakilisha watu wenye ulemavu kutoka Rwanda,Alex Bahati ambaye amewasilisha hoja inayolenga kuhimiza Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi wanachama kutekeleza hatua zinazohitajika ili kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu.
Akielezea madhumuni ya hoja hiyo, Mbunge Alex amesema inakusudia kuiwezesha Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa maelekezo kwa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo na nchi wanachama kuhakikisha mahitaji ya watu wenye ulemavu yanazingatiwa katika utekelezaji wa sera, mipango na utoaji wa huduma.
Amesema hoja hiyo inasisitiza umuhimu wa kutekeleza dhana ya reasonable accommodation, inayomaanisha kufanya marekebisho yanayofaa na kutoa msaada unaohitajika ili watu wenye ulemavu waweze kutumia haki na fursa zao kwa usawa na watu wengine.
“Marekebisho hayo yanajumuisha kuweka miundombinu inayofikika, ikiwemo lifti katika majengo, pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa watu wenye matatizo ya kusikia na mahitaji mengine yanayotokana na aina mbalimbali za ulemavu.”amesema Alex .
Alex ameongeza kuwa ,hatua hizo zinapaswa kuzingatia mahitaji ya kila mtu mwenye ulemavu ili kuhakikisha kuwa hakuna anayezuiwa kupata huduma au kushiriki katika shughuli za kila siku kutokana na vikwazo vinavyoweza kuondolewa.
Ameongeza kuwa, ni muhimu kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka juhudi za pamoja katika kuhakikisha dhana hiyo inatekelezwa, badala ya kubaki katika maandishi na matamko yasiyoleta mabadiliko katika maisha ya watu wenye ulemavu.
Aidha, ameeleza kuwa Muswada wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu (Persons with Disabilities Bill), ambao umekuwa ukichelewa kupitishwa, unaendelea na hatua zinazohitajika, huku akieleza matarajio ya kupitishwa kwake katika kikao cha Bunge kinachotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Alex amesema kupitishwa kwa sheria hiyo kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya kisheria inayolenga kulinda haki za watu wenye ulemavu na kuweka msingi wa kushughulikia changamoto zinazowakabili katika kupata huduma na kushiriki katika maendeleo ya jamii.
Hoja hiyo inalenga kuhamasisha taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na serikali za nchi wanachama kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa hatua zinazohakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao na kushiriki katika maendeleo kwa usawa na wananchi wengine.

