Na, WMJJWM, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha waendesha bodaboda nchini kuimarisha shughuli zao za kiuchumi, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya Taifa.
Maswi ameyasema hayo, Oktoba 19, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na viongozi na wawakilishi wa waendesha bodaboda kutoka mikoa ya Dodoma, Dar Es Salaam, Morogoro, Tanga, Singida, Arusha na Njombe, katika kikao kilicholenga kujadili mbinu za kuimarisha sekta hiyo na kuweka mikakati ya kuwawezesha madereva kiuchumi.
Amesema waendesha bodaboda ni sehemu muhimu ya jamii na uchumi wa Taifa, kutokana na mchango wao katika kutoa huduma za usafiri, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kujiajiri na kutoa fursa za ajira kwa vijana na wananchi wengine.
“Ninachoomba kwenu ni kuiona sekta ya usafiri wa bodaboda inakuwa na hadhi, madereva wenye weledi na uwezo wa kujiongezea kipato, kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla,” amesema Maswi.
Maswi amesema Serikali imeanzisha programu tumizi ya Jamii Wezesha, inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na fursa za uwezeshaji wa kiuchumi kwa wafanyabiashara ndogondogo nchini.
Amesema mpango huo unalenga kutumia teknolojia kurahisisha utambuzi na usajili wa wafanyabiashara ndogodogo wakiwemo waendesha bodaboda, ili kuwasaidia kufahamu na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazopatikana kupitia mifumo na programu ya Jamii Wezesha.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Waendesha Pikipiki Tanzania (CHAWAPITA), Daudi Laurian amesema bado kuna umuhimu wa jamii kubadili mitazamo hasi kuhusu waendesha bodaboda na kutambua mchango wao katika uchumi wa familia na Taifa.
Ameeleza kuwa elimu ya uwekezaji na utunzaji wa fedha ni muhimu kwa madereva hao ili kuwasaidia kutofautisha mahitaji muhimu na matumizi yasiyo ya lazima, kuweka akiba na kuanzisha miradi itakayowaongezea kipato kwa muda mrefu.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na viongozi wa waendesha bodaboda, kutambua changamoto zinazowakabili na kujadili njia zinazoweza kusaidia kuboresha mazingira yao ya kazi na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

