Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mheshimiwa Hakainde Hichilema, amesisitiza umuhimu wa nchi za Jumuiya za Ukanda wa Maziwa Makuu kuimarisha umoja na mshikamano katika kutafuta suluhu ya migogoro inayoukabili Ukanda huo, huku zikiwekeza zaidi katika kukuza uchumi, biashara na uwezo wake wa kujitegemea kiuchumi kupitia rasilimali zake

Rais Hichilema ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Kamati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (RIMC), uliofanyika jijini Lusaka, nchini Zambia, tarehe 19 Oktoba, 2026.

Aidha Mheshimiwa Hichilema, amesisitiza umuhimu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kutumia mifumo yake na uwezo wa ndani kutatua changamoto zinazowakabili, badala ya kutegemea kwa kiasi kikubwa nguvu kutoka nje ya Ukanda huo. Aidha, amehimiza nchi za Maziwa Makuu kuimarisha uwekezaji, biashara na ushirikiano wa kiuchumi ili kukuza uchumi wa bara na kuongeza manufaa kwa wananchi wake kama njia mbadala ya kutatua migogoro inayowakabili.

Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kwa lengo la kujadili masuala ya amani, usalama na ushirikiano wa kikanda, pamoja na kutafuta njia endelevu za kuhakikisha amani ya kudumu katika Ukanda huo.

Tanzania inashiriki mkutano huo kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ambaye anawakilisha nchi katika majadiliano yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na juhudi za pamoja za kudumisha amani na usalama.

Viongozi wengine walioambatana na Mheshimiwa Waziri Kombo katika mkutano huo ni pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Mhandisi Cyprian John Luhemeja, Mkuu wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ali Bujiku pamoja na viongozi na maofisa wengine kutoka taasisi mbalimbali za serikali.

Jumuiya ya ICGLR ni jukwaa la kikanda linalolenga kukuza amani, usalama, utulivu na maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Ushirikiano wa nchi wanachama ni muhimu