Na Silivia Amandius – Karagwe

Zaidi ya wananchi laki tatu katika mji wa Kayanga na vijiji 29 vya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera wanatarajiwa kunufaika na mradi mkubwa wa maji wenye gharama ya shilingi bilioni 64, ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 79.82.

Mradi huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, huku ukitarajiwa kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwa Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, Mhandisi Evodius Beyange kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), amesema utekelezaji wa mradi unaendelea, huku maendeleo ya kifedha yakifikia asilimia 72 na mkandarasi akiwa tayari amelipwa shilingi bilioni 44.

Amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi Afcon kwa kushirikiana na Vijeta, huku kampuni ya WAPCOS ikiwa mshauri wa mradi. Miundombinu inayojengwa inajumuisha chanzo cha maji, mabomba ya kusafirisha maji, mtambo wa kutibu maji pamoja na tanki la kuhifadhi maji kabla ya kusambazwa kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Beyange, kazi zilizofanyika katika chanzo cha maji ni pamoja na ujenzi wa jengo la pampu na ufungaji wa pampu tatu. Hata hivyo, kazi ya kulaza bomba kuu kutoka kwenye jengo la pampu hadi ziwani pamoja na baadhi ya kazi za umeme bado zinaendelea.

Ameongeza kuwa ujenzi wa mtambo wa kutibu maji umefikia asilimia 72, huku miundombinu 26 iliyopangwa kujengwa katika eneo hilo ikiwa tayari imejengwa na kazi za umaliziaji zikiendelea. Kazi hizo ni pamoja na ufungaji wa pampu za maji yaliyotibiwa na kukamilisha jengo la vichujio.

Aidha, tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano za maji limefikia hatua za mwisho za utekelezaji, huku kazi zilizobaki zikihusisha umaliziaji wa baadhi ya miundombinu na mandhari ya eneo hilo.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, mmoja wa viongozi waliohusika na ziara hiyo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji, akisema mradi huo utasaidia kukidhi mahitaji ya maji ya wananchi na wafanyabiashara.

Amesema upatikanaji wa maji ya uhakika utakuwa chachu kwa shughuli za kiuchumi, zikiwemo biashara za mama lishe, hoteli, migahawa na viwanda, ambavyo vinahitaji maji kwa ajili ya uzalishaji na utoaji wa huduma.

Mradi huo unatarajiwa kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kayanga na vijiji vinavyolengwa, kuongeza fursa za kiuchumi na kuimarisha ustawi wa jamii pindi utakapokamilika na kuanza kutoa huduma.