Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Wilaya ya Mbagala, Jeremiah Jahulula leo Oktoba 16, 2026 Jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mradi wa kufunga Transforma 10, Kata ya Kijichi ikiwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa umeme iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Kata hiyo 

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Said Mremi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho ya miundombinu ya umeme katika mkoa huo.

Mafundi wa TANESCO Wilaya ya Mbagala wakifunga Transforma katika Kata ya Kijichi

………..

Shirika la Umeme Tanzania (TNESCO), Wilaya ya Mbagala, limeanza kufunga Transforma 10 katika Kata ya Kijichi, Manispaa ya Temeke, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa umeme iliyokuwa ikiwakabili wananchi, kutokana na ongezeko la mahitaji ya umeme.

Akizungumza Oktoba 16, 2026, jijini Dar es Salaam, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Mbagala, Jeremiah Jahulula, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili, hatua itakayosaidia kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wakazi wa kata ya kijichi.

Mhandisi Jahulula amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya shirika kupokea taarifa za wateja kuhusu kutokidhi kwa mahitaji ya umeme, hivyo kuamua kufanyia kazi changamoto hiyo ili kuboresha huduma kwa wananchi.

“Mradi huu ni sehemu ya jitihada endelevu za TANESCO Wilaya ya Mbagala katika kutatua changamoto zinazowakabili wateja wetu. Pia natoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme,” amesema
Mhandisi Jahulula.

Mhandisi Mkuu wa TANESCO Wilaya ya Mbagala, Emmanuel Nzuki, amesema kuwa eneo hilo lilikuwa na uwezo wa megawati tano, lakini kupitia maboresho yanayoendelea, uwezo huo utaongezeka kwa megawati 2.5 na kufikia megawati 7.5 ili kukidhi mahitaji ya wateja.

Amesema ongezeko hilo linatokana na ujenzi wa laini mpya ya umeme ya kilovolti 33, itakayounganishwa na laini iliyopo ya kilovolti 11, hatua inayolenga kuimarisha usambazaji wa umeme na kupunguza changamoto zinazotokana na ongezeko la matumizi ya nishati hiyo.

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Said Mremi, amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za shirika kuboresha huduma kwa wateja na kutatua changamoto za upatikanaji wa umeme. Huku akiwataka wananchi kulinda miundombinu ya umeme na kutoa taarifa wanapobaini hitilafu kwa kupiga simu kupitia namba ya huduma kwa wateja isiyolipiwa, 180.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtoni Kijichi, Mohamed Rajabu, ameishukuru TANESCO kwa kuchukua hatua kutatua changamoto ya upungufu wa umeme, akisema hali hiyo ilikuwa ikiwapa usumbufu wananchi kwa muda mrefu.