Na Silivia Amandius
Ngara, Kagera.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta chanzo kipya cha maji kwa ajili ya wananchi wa Kata ya Kabanga, Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika.
Akizungumza na wananchi wa Kabanga, Mhandisi Kundo amesema Serikali inatekeleza mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 120 katika kata hiyo, huku mradi mwingine wa shilingi milioni 300 ukiwa tayari umetekelezwa. Amesema Serikali pia itafanyia kazi changamoto ya mabomba ya zamani yanayopasuka na kusababisha upotevu wa maji.
Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda vyanzo vya maji na miundombinu ya miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu, akisisitiza kuwa fedha zinazotumika kutekeleza miradi ya maendeleo zinatokana na kodi za wananchi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma ya maji safi na salama katika vijiji mbalimbali nchini, akieleza kuwa upatikanaji wa maji utasaidia kuboresha maisha ya wananchi, kupunguza changamoto za majumbani na kuchochea shughuli za kiuchumi katika jamii.

