Mkurugenzi wa shule za Nakido, Haruna Kakiva akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha

Meneja wa Latra mkoa wa Arusha Omar Ayoub akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha

Na Happy Lazaro, Arusha.
Mkurugenzi wa shule za Nakido, Haruna Kakiva, amesema shule hiyo imeendelea kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kielimu kwa wanafunzi waliokuwa na matokeo duni, kwa kuwasaidia kuboresha ufaulu wao na kuendelea na safari ya elimu hadi vyuo vikuu.
Ameyasema hayo jijini Arusha katika mahafali ya 11 ya shule ya sekondari Nakido, ambapo jumla ya wanafunzi 92 wamehitimu.
Kakiva amesema shule hiyo imewahi kupokea wanafunzi waliopata alama za D na kukosa nafasi katika baadhi ya shule za serikali, lakini kupitia juhudi za walimu na usimamizi mzuri, wameweza kuhitimu kidato cha nne wakiwa wamefaulu.
Amesema siri ya mafanikio hayo ni kuweka mkazo katika ufundishaji bora sambamba na kujenga nidhamu kwa wanafunzi, walimu na viongozi wa shule, akieleza kuwa elimu bila nidhamu haiwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Kakiva ameongeza kuwa shule hiyo imeweka utaratibu wa kuwajibishana pale mtu anapokiuka kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Shule inawaandaa wanafunzi kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili unde (AI), ambayo yanaendelea kubadilisha namna watu wanavyofanya kazi.”amesema Kakiva .
Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kujifunza kuitumia teknolojia hiyo kwa tija ili iwe nyenzo ya kuwaongezea uwezo badala ya kuwafanya washindwe kukabiliana na ushindani wa maisha..
Amesema wahitimu wa shule hiyo wameendelea kujiunga na shule mbalimbali nchini na wengi wamefanya vizuri katika masomo yao, huku baadhi wakifanikiwa kufika vyuo vikuu.
Kakiva ameongeza kuwa mrejesho unaotolewa na wazazi na wahitimu wanaorejea shuleni kueleza maendeleo yao ni motisha kwa uongozi kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Aidha Kakiva amewataka wazazi kujenga ukaribu na watoto wao kwa kuwa marafiki wanaoweza kuwaeleza changamoto, furaha na mambo yanayowatatiza.
“Dunia ya sasa ina mabadiliko ya haraka, hivyo wazazi wanapaswa kufahamu kile watoto wao wanachokutana nacho ili kuwaongoza kutambua fursa na kuepuka mambo yanayoweza kuhatarisha maisha na maendeleo yao.”amesema Kakiva.
Aidha, amewashauri wahitimu kuendelea kudumisha nidhamu waliyojifunza shuleni, kuwaheshimu na kuwapenda wazazi wao pamoja na kuwa na bidii katika masomo wanapojiandaa kuingia katika hatua nyingine za elimu.
“Uongozi wa shule utaendelea kusimamia misingi ya elimu, nidhamu na uwajibikaji kwa lengo la kuwajenga vijana wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.”amesema Kakiva.
Kwa upande wa mgenirasmi katika mahafali hayo ,Meneja wa Latra mkoa wa Arusha ,Omar Ayoub amesema baada ya kuhitimu Kidato cha Nne, wanafunzi wanapaswa kufanya uchaguzi sahihi wa masomo au vyuo kulingana na taaluma wanazotaka kusomea, akitoa mfano kuwa mwenye ndoto za kuwa mhandisi anapaswa kuchagua chuo kinachotoa mafunzo ya uhandisi, huku anayetaka kuwa mhasibu akichagua taasisi inayotoa mafunzo ya uhasibu.
Aidha amewataka wahitimu hao kujiendeleza zaidi kwani kidato cha nne ni mwanzo tu wa elimu hivyo wanatakiwa kuongeza bidii zaidi katika kujituma kwa kwenda viwango vingine ili waweze kufikia ndoto zao .
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Shule Mhandisi David Mtunguja, amewataka wahitimu wa Kidato cha Nne kuchagua njia za kuendeleza elimu yao kwa kuzingatia ndoto na malengo waliyojiwekea badala ya kufuata mkumbo.
Amesema elimu ni mchakato unaomsaidia mtu kufikia ndoto zake, huku elimu ya sekondari ikiwa ni hatua muhimu ya mwanafunzi kujitambua, kutambua uwezo wake na kuamua anataka kuwa nani katika maisha yake ya baadaye.
