*Lengo ni kuchochea utekelezaji wa shughuli za madini kwa kuzingatia weledi

*Kamati yaipongeza serikali,yasisitiza ukamilishaji wake wa haraka

Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato wa kisheria utakaowezesha kuundwa kwa Bodi ya Usajili na Udhibiti wa Wajiolojia nchini hatua hiyo inalenga kusimamia maadili, kuweka viwango vya kitaaluma, na kuondoa vishoka pamoja na wataalamu wasio waaminifu wanaoipotezea fedha serikali na wawekezaji kwa kutoa taarifa zisizo sahihi za jiosayansi.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 15,2026 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akiwasilisha taarifa ya Mpango wa kuwainua na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Waziri Mavunde amesema kuwa, taratibu za ndani za serikali zinaendelea juu ya mapendekezo wa muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wajiosayansi kwa ajili ya hatua zake muhimu za kupitishwa.

Mavunde ameieleza Kamati kuwa, bodi hiyo itakuwa na mamlaka kamili ya kuratibu taaluma hiyo, kusajili wataalamu wenye sifa, na kuhakikisha ripoti zote za utafiti zinazotolewa nchini zinabeba uwajibikaji wa kisheria.

Ameongeza kuwa, Kuanzishwa kwa chombo hiki kunakuja kama tiba ya kilio cha muda mrefu cha Jumuiya ya Wanajiolojia Tanzania (TGS) ambapo kwa miaka mingi, sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya watu wasio na sifa kufanya tafiti za miamba na madini, jambo linalosababisha wachimbaji wadogo na wawekezaji kupoteza mitaji mikubwa kwa kufanya uchimbaji wa kubahatisha kutokana na taarifa zisizo sahihi.

Akielezea kuhusu manufaa kwa Wawekezaji na Wachimbaji, Mavunde amefafanua kuwa, Ujio wa bodi hii unatarajia kuleta mageuzi makubwa katika sekta, kwasababu kupitia ripoti ya utafiti iliyoidhinishwa na bodi mchimbaji atakuwa na fursa ya kuwasilisha katika taasisi za fedha ili kupata mkopo au kwa mwekezaji wa nje ambayo itakuwa na muhuri rasmi wa mtaalamu anayetambulika na kuwajibika kisheria.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Simon Songe ameeleza kuwa, kamati ya Bunge imeamua kuweka suala hili kama kipaumbele chake cha kwanza katika kuendeleza na kuimarisha Sekta ya Madini ili kulinda taswira ya nchini hususan kwa wawekezaji na wachimbaji wadogo ambao kwasasa wanamchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

Sambamba na hapo, kamati imeendelea kuipongeza wizara ya madini na taasisi zake kwa kazi nzuri inayofanya kuanzia katika usimamizi na utekelezaji wa vipaumbele vyake ilivyopangwa katika Mwaka wa Fedha 2026/2027.