Na Silivia Amandius- Kagera.
Kampeni ya Pika Smart awamu ya pili imezinduliwa mkoani Kagera kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia umeme kama nishati safi, salama na nafuu ya kupikia, hatua inayotarajiwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kulinda afya za familia na kuhifadhi mazingira.
Kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za kupikia kwa umeme pamoja na kuwapatia fursa ya kupata majiko ya umeme kwa gharama nafuu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kufikia lengo la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ifikapo mwaka 2034.
Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Ramadhani Kido, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga, alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kitaifa inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alieleza kuwa matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kulinda afya za wananchi, kupunguza gharama za uendeshaji wa kaya, kuhifadhi mazingira na kuokoa muda wa familia, hususan wanawake ambao mara nyingi hutumia muda mwingi kutafuta kuni na kuandaa chakula kwa kutumia nishati zinazozalisha moshi.
Nyamahanga alisema Mkoa wa Kagera unaendelea kutekeleza ajenda hiyo kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika kaya na taasisi zinazohudumia watu wengi. Aliongeza kuwa kuunganishwa kwa umeme katika vijiji vya mkoa huo kumeweka mazingira wezeshi kwa wananchi kutumia umeme katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kupikia.
Alisisitiza kuwa Serikali inapohamasisha wananchi kupikia kwa umeme haizungumzii mipango ya baadaye pekee, bali inahimiza matumizi sahihi ya miundombinu ya umeme ambayo tayari imewekezwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Kupitia uzinduzi huo, aliwataka wananchi kutumia umeme si kwa ajili ya mwanga pekee, bali pia kupikia ili kupunguza athari za moshi unaotokana na kuni na mkaa, ambao unaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji, hasa kwa wanawake na watoto.
Aidha, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, aliwaelekeza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na viongozi wengine kuhakikisha elimu kuhusu matumizi ya umeme kupikia inawafikia wananchi hadi ngazi ya vijiji, huku wakitoa mwongozo kuhusu matumizi salama na yenye ufanisi.
Kwa upande wake, balozi wa kampeni hiyo kutoka Tanzania House of Talent (THT), Mrisho Mpoto, alisema kampeni hiyo inaungwa mkono na Serikali na kufadhiliwa na mradi wa Modern Energy Cooking Services (MECS) kupitia Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza.
Mpoto alieleza kuwa kampeni hiyo inatekelezwa na THT Innovation Limited kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Alisema kampeni hiyo itafanyika katika mikoa saba nchini, ikihusisha mikutano ya uhamasishaji na maonesho ya vifaa vya kupikia kwa umeme, pamoja na kuwawezesha wananchi kupata majiko hayo kwa gharama nafuu kupitia mifumo ya malipo inayolenga kupunguza changamoto ya gharama za awali.
Naye Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Lilian Mgai, alisema shirika hilo limeweka utaratibu wa kuwawezesha wananchi kupata majiko ya umeme na kulipia gharama zake kidogo kidogo kupitia manunuzi ya umeme wa LUKU hadi deni litakapokamilika.
“Gharama za kuanzia imekuwa ni mojawapo ya vikwazo vikubwa vya kupika kwa umeme. TANESCO, kupitia mradi wa On-Bill Financing, mteja anaweza kuchukua jiko la umeme leo na kulilipia kidogo kidogo kila anaponunua LUKU,” alisema Mungai.
Aliwahimiza wananchi wa Kagera kutembelea ofisi za TANESCO kwa ajili ya kupata maelekezo na kujiunga na mpango huo, akieleza kuwa utaratibu huo utasaidia kupunguza kikwazo cha gharama za awali na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kampeni ya Pika Smart inatarajiwa kuchangia juhudi za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kupunguza ukataji wa miti na kuimarisha utunzaji wa mazingira, sambamba na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama katika kaya za Watanzania.

