Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
15,oktoba 2026
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumpokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anayetarajiwa kufanya ziara mkoani humo Oktoba 16, 2026, itakayohusisha kutembelea miradi ya uwekezaji na maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu anatarajiwa kutembelea eneo la kongani ya uwekezaji la Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), lililopo Zinga, wilayani Bagamoyo, kwa ajili ya kukagua shughuli za uwekezaji na ujenzi wa viwanda.
Aidha, anatarajiwa kutembelea Mbegani kukagua ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na baadaye kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo, wilayani Bagamoyo.
Ziara hiyo inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya uwekezaji na maendeleo pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kuwasilisha maoni na masuala mbalimbali yanayowahusu.
