Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka Mawaziri na watendaji wa Serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa Watanzania wanahitaji huduma za uhakika za maji, umeme na barabara badala ya kuendelea kusikiliza ahadi.
Makamu wa Rais ametoa msisitizo huo wakati akizungumza na wananchi wa Tunduma mkoani Songwe, waliojitokeza kumpokea akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo, ambapo ametumia fursa hiyo kutoa maelekezo ya moja kwa moja kwa Mawaziri alioambatana nao akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ujenzi na Nishati.
Katika hatua hiyo, Mhe. Ndejembi amewataka viongozi wanaosimamia sekta ya maji kuhakikisha wanaharakisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Tunduma, akieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari ametoa Malipo ya awali ya Mradi Mkubwa wa maji Tunduma, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuchelewa.
Akizungumzia sekta ya Nishati, Makamu wa Rais ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha ahadi ya kuwasha umeme katika Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Nkangamo ifikapo Desemba mwaka huu inatekelezwa, ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe, hususani Tunduma, na kuchochea shughuli za uzalishaji na biashara.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amemwelekeza Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, kuongeza usimamizi kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa barabara katika eneo hilo, ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ifikapo Oktoba 31, 2026, kama ilivyoahidiwa, badala ya wananchi kuendelea kuathiriwa na ucheleweshaji wa ujenzi.
Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa Serikali ina mipango mingi na mizuri ya maendeleo, lakini mafanikio yake yanategemea uwajibikaji, usimamizi madhubuti na utekelezaji unaozingatia muda, akieleza kuwa kipimo cha utendaji wa viongozi ni matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
Aidha, amesisitiza kuwa maendeleo hayana itikadi, au asili ya mtu anapotokea, isipokuwa wananchi wote wanahitaji kupata huduma bora, hivyo amewataka viongozi kuweka mbele maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Awali, kabla ya kuzungumza na wananchi hao, Makamu wa Rais alitembelea Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Nkangamo, kilichopo Momba mkoani Songwe, kinachojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 285.7, ikiwa ni sehemu ya miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha miundombinu ya nishati nchini na kufungua fursa za biashara ya umeme katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kupokea umeme wa msongo wa kilovolti 400 na kuushusha katika viwango vya kilovolti 330, 220 na 33, hatua itakayowezesha kuimarisha usambazaji wa umeme kwa matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwa Makamu wa Rais na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, hadi Oktoba 11, 2026, utekelezaji wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 83.13, huku uwashaji wa umeme katika kituo hicho ukitarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa nishati katika Mkoa wa Songwe, kuchochea ukuaji wa viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, pamoja na kuiwezesha Tanzania kushiriki katika biashara ya kuuziana umeme na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nishati ya Kusini mwa Afrika (SAPP), kupitia Zambia, baada ya nchi hiyo kukamilisha sehemu yake ya mradi wa TAZA.
Ziara hiyo ya Makamu wa Rais mkoani Songwe imelenga kukagua miradi ya Maendeleo inayoendelea kutekelezwa mkoani Songwe katika kuhakikisha kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatafsiriwa kuwa huduma halisi zinazoboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Halmshauri ya Mji wa Tunduma, akiwa Ziarani Mkoani Songwe, leo tarehe 15 Oktoba 2026.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasalimu wananchi mbalimbali wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma waliojitokeza kumpokea wakati akiingia Mkoa wa Songwe kwa Ziara ya kikazi, tarehe 15 Oktoba 2026.






