Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ramadhan Kimara, amekamata gari (lori)lililokuwa likisafirisha mchanga bila kuwa na risiti ya malipo ya ushuru, katika hatua ya kudhibiti upotevu wa mapato ya halmashauri hiyo.

Kimara amekamata gari hilo wakati wa ziara ya kukagua vyanzo vya mapato katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, akifuatilia utekelezaji wa taratibu za ukusanyaji wa ushuru.

Katika ziara hiyo, amefuatilia utendaji wa watumishi wenye dhamana ya kukusanya mapato ili kuhakikisha ushuru unaolipwa unaingizwa na kurekodiwa katika mfumo rasmi wa halmashauri.

Kimara alisema,ukaguzi huo unalenga kubaini mianya ya upotevu wa mapato na kuhakikisha kila shughuli inayopaswa kulipiwa ushuru inafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, hatua hiyo inayoonesha kuendelea kufanya ufuatiliaji wa mapato ili kuinua mapato ya Halmashauri.

Halmashauri hiyo inaendelea kuimarisha usimamizi wa vyanzo vyake vya mapato na uwajibikaji wa watendaji ili kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinasaidia kuboresha huduma za kijamii na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Kibiti.