Leo ni kumbukizi ya baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Mwandishi wetu
Ni miaka 27 ya kumbukizi, na Sekta ya Maji katika kumbukizi hii inajipambanua kuwa moja ya wachangiaji wakubwa katika kuondosha wajinga ambao Mwal. Julius Nyerere alivalia njuga kila kukicha, yaani Ujinga, Umasikini na Magonjwa. Huduma yam aji inawafikia wananchi na kuondosha muda mwingi unaotumika kutafuta maji, na mashuleni kuleta utulivu kwa wanafunzi. Wanafunzi wanapata mud awa kusoma na kufaulu vizuri.
Pamoja na hilo, huduma imeondosha maradhi yaliyosababishwa na matumizi yam aji yasiyokuwa safi na salama. Majisafi na salama yameokoa kiwango kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kutibu wananchi. Kadhalika, maji yanatumika kusisimia huduma nyingine za uchumi na kuongeza ubora wa bidhaa mbalimbali, hivyo kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Maji ni injini ya uchumi kwa ujumla.
Sekta ya Maji imeendelea kupata mafanikio katika maeneo mbalimbali muhimu, yakiwemo, kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya maji ni juhudi zinazoendelea za Serikali katika kuongeza wigo wa huduma na kuwafikisha huduma kwa wananchi maji safi na salama.
Hivi sasa upatikanaji wa huduma ya maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 83.0 mwaka 2024 hadi asilimia 85.2 mwaka 2025, na mijini huduma imeongezeka kutoka asilimia 91.6 hadi asilimia 92.5. Pamoja na hilo, jumla ya vijiji 10,758 kati ya vijiji 12,333 vimefikiwa na huduma ya maji ya uhakika.
Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vilivyosalia 1,575 , kwa lengo la kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma na kuhakikisha idadi kubwa ya wananchiinafikiwa. Katika kuhakikisha miradi ya maji mijini na vijijini inatekelezwa kwa wakati na kuleta matokeo kusudiwa kwa wananchi, Serikali imeongeza bajeti ya Sekta ya Maji kutoka Shilingi 898,276,453,000.00/= hadi kufika Shilingi 1,120,194,614,000/=. Hatua hii itawezesha kutekeleza miradi 1,188 midogo na miwili mikubwa. Fedha hizo zitatumika kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji pamoja na ubora wake.
Pamoja na hilo, kuanza utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 340 visivyokuwa na huduma ya maji kati ya jumla ya vijiji 1,575 visivyokuwa na huduma ya maji na katika kuhakikisha huduma ya maji inafika katika vijiji vyote nchini, Serikali katika mwaka 2026/27, imeanza utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 400 kati ya vijiji 1,575 ambavyo havina huduma ya maji.
Hatua hii inalenga kuongeza kasi ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama, hususan katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu na huduma hiyo ambapo jumla ya wananchi 1,440,256 watanufaika katika vijiji hivyo 400.
Pia serikali imeanza na kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa lengo lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji na upatikanaji wa maji, kuimarisha uhakika wa huduma na kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyo vya uhakika. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa bwawa la Kidunda,ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 329.47 na utekelezaji wake hadi Septemba, 2026 umefika asilimia 65.7.
Ujenzi wa Bwawa la Farkwa, kwa ajili ya kuongeza upatikanaji na uhakika wa huduma ya maji katika Jiji la Dodoma na maeneo yanayolizunguka. Mradi huo una thamani ya takribani Shilingi bilioni 312 . Bwawa hilo linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 400 ,
Mradi wa maji kutoka mto Rufiji kwenda Dar es Salaam na Pwani ambapo Wizara ya Maji imekamilisha upembuzi yakinifu wa mradi wa kuchukua maji kutoka mto Rufiji na kuyapeleka katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani. Lengo ni kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ongezeko la watu, shughuli za kiuchumi na upanuzi wa maeneo ya makazi. Kwa sasa kazi inayoendelea ni kufanya usanifu wa kina wa mradi huo utakaobainisha gharama na miundombinu itakayojengwa.
Miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji, ni mpango wa kimkakati wa kitaifa wa muda mrefu unaolenga kuunganisha vyanzo vikuu vya maji nchini kupitia mtandao . miundombinu ya usafirishaji wa maji kwa wingi (bulk water transmission network). Mpango huo unahusisha vyanzo vikuu vya maji vya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, Mto Rufiji, Mto Ruvu, Mto Pangani, Mto Wami, Mto Kagera, Mto Malagarasi, Mto Great Ruaha pamoja na mabwawa makubwa ya kimkakati kama vile Bwawa la Julius Nyerere, Bwawa la Kidunda, Bwawa la Farkwa na mabwawa mengine yatakayojengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa sasa maandalizi na usanifu unaendelea kwa miradi inayohusisha; maji kutoka ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida; maji kutoka ziwa Tanganyika kwenda Kigoma, Katavi na Rukwa; maji kutoka ziwa Nyasa kwenda maeneo ya Ruvuma, Mtwara na Njombe; maji kutoka mto Rufiji kwenda Dar es Salaam na Pwani; na miradi mingine inayounganisha vyanzo vikubwa vya maji na maeneo yenye mahitaji.
Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika maeneo ya vijijini kwa lengo la kuongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma ya maji ya uhakika. Miongoni mwa maeneo yenye miradi ya kuimarisha huduma ni pamoja na mradi wa maji Ruangwa, Lindi na Nachingwea ambapo Serikali na inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Nyangao uliopo Wilaya ya Lindi kwenda Wilaya tatu) za Lindi, Ruangwa na Nachingwea kwa gharama ya Shilingi bilioni 119.56.
Mradi unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha kupeleka maji kwenye vijiji 29 vya Wilaya hizo ambapo Ruangwa ni vijiji 25, Nachingwea vitatu (3) na kijiji kimoja (1) katika Wilaya ya Lindi. Hadi mwezi Septemba 2026, utekelezaji umefika asilimia 77. Utekelezaji wa awamu ya pili utaanza baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza na utahusisha jumla ya vijiji 27 ambapo vijiji tisa (9) ni vya Wilaya ya Ruangwa; na vijiji 18 Wilaya ya Nachingwea.
Tanzania tunaweza kusema safari kuhusu tulipotoka ni mbali na tunapoenda ni karibu zaidi katika huduma ya maji kwa wananchi. Serikali inaendelea kKuhakikisha idadi ya vijiji vyote 1,575 visivyokuwa na huduma ya maji vinapata huduma hiyo, ambapo kati ya vijiji hivyo katika mwaka 2026/27 vijiji 400 vitapata huduma ya maji. Pia, utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji na kuunganisha vyanzo vya uhakika na maeneo yenye mahitaji. Kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika uwekezaji katika Sekta ya Maji pamoja na kukamilisha Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji (National Water Master Plan) ikiwa ni nyenzo muhimu ya kupanga maendeleo ya rasilimali za maji kwa muda mrefu.
Pamoja na hayo kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji, kuimarisha usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za maji, pamoja na kuwekeza katika ubunifu, sayansi na teknolojia ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa ubora, uhakika na uendelevu.
