Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amewahimiza vijana kutumia fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuendeleza vipaji vyao na kutimiza ndoto zao.
Prof. Mkenda ameyasema hayo jana, tarehe 10 Oktoba 2026 wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Vijana Kitaifa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Profesa Mkenda amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu na Mafunzo ya ufundi stadi, mafunzo ya uanagenzi na uzoefu kazini ili kuwaandaa vijana kukidhi mahitaji ya soko la ajira sambamba na kuweka mifumo inayorahisisha upatikanaji wa taarifa, mitaji na masoko.
Ameongeza kuwa juhudi za kujenga vyuo vya VETA katika kila wilaya zinalenga kupanua upatikanaji wa mafunzo hayo na kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kuanzisha biashara, kutumia teknolojia na kushiriki katika maendeleo ya taifa.
“Kwa Tanzania, tunafundisha ufundi kwa lugha ambayo mwanafunzi anaweza kuimudu. Ukienda VETA na unataka kufundishwa kwa Kiswahili, utafundishwa kwa Kiswahili; ukitaka Kiingereza, utafundishwa kwa Kiingereza. VETA haiwezi kumfelisha mwanafunzi kwa sababu tu hajui Kiingereza,” amesema.
Akiwa katika banda la VETA wakati wa kutembelea mabanda ya maonesho ya Wiki hiyo, Prof. Mkenda alifurahishwa na uwezo na umahiri wa vijana wenye ulemavu kutoka vyuo mbalimbali vya VETA na kutumia fursa hiyo kuhimiza vijana wengine wenye ulemavu kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA ili kujikwamua kiuchumi na kufafanua kuwa Serikali inagharamia ada kwa kundi hilo.
“Ukijiunga kwenye vyuo vya VETA, Serikali inagharamia kulipa ada ya mafunzo yako. Kwa hiyo vijana wengine wenye ulemavu wahamasike kujiunga,”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Abdallah Ngodu, amesema kaulimbiu ya maonesho hayo, “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana,” inaakisi jukumu la taasisi hiyo la kutoa mafunzo bila ubaguzi.
Amewahimiza vijana na wananchi kujiunga na kozi za VETA, akieleza kuwa dirisha la udahili wa kozi za muda mrefu limeongezewa mpaka tarehe 20 Oktoba 2026.

