Sumbawanga, Rukwa.

Kuelekea kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2026 ambazo zinatanguliwa na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika mkoani Rukwa, Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Chacha Mwita Moseti amewakaribisha wananchi kutoka ndani na nje ya Mkoa huo kutembelea Banda la TARURA ambao wanashiriki katika maadhimisho hayo ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga.

Mhandisi Moseti amesema kuwa TARURA inashiriki maadhimisho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake sambamba na kupokea kero na malalamiko moja kwa moja kutoka kwa wananchi na kuyapatia majawabu. 

Ameongeza kuwa pamoja na kutoa elimu, TARURA pia inayatumia maadhimisho hayo kueleza teknolojia mbalimbali inazozitumia katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, ushirikishwaji wa jamii hususani vijana katika matengenezo madogo madogo ya barabara (CBRM) pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya barabara na kuchukua tahadhari wakati wa matumizi ya barabara kuelekea msimu wa mvua ambazo zinatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Uzinduzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana 2026 utafanyika tarehe 10 Oktoba, 2026 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Mazingira tofauti, fursa sawa kwa Vijana”.

Maadhimisho hayo ya Wiki ya Vijana Kitaifa yatafuatiwa na Sherehe za uzimaji wa Mwenge wa Uhuru 2026 zitakazoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 14 Oktoba, 2026 katika Uwanja wa Nelson Mandela, Mjini Sumbawanga. 

Sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru zinaenda sambamba na kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Julius Kambarage Nyerere aliyefariki Oktoba 14, 1999.