Kigoma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Kigoma imesaini mikataba na Vikundi vya Kijamii (CBGs) ishirini na tatu (23) kwa lengo la kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara za wilaya hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 201.4 kwa mwaka.
Hafla ya utiaji saini imefanyika leo tarehe 09 Oktoba 2026 kwa vikundi 18 kutoka Manispaa ya Kigoma/Ujiji na vikundi 5 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Dkt. Rashid Chuachua amewataka wanachama wa vikundi hivyo kusimamia usafi na usalama wa barabara huku akiwataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao hususan hifadhi ya barabara.
Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Kigoma Mhandisi Goodluck Mbanga amesema katika mkoa huo ni wilaya mbili tu zinazotekeleza shughuli hizo ambazo ni Kigoma na Kakonko hivyo amevitaka vikundi hivyo vya mfano kufanya vizuri katika shughuli za matengenezo ya kawaida ya barabara ili wilaya zote za mkoa wa Kigoma ziweze kutekeleza shughuli za CBRM.
Aidha, amesema kwa wilaya ya Kigoma jumla ya barabara zenye urefu kilomita 122.02 zitahudumiwa na vikundi vya kijamii vilivyosaini mikataba.
Wakati huo huo, Meneja wa TARURA wilaya ya Kigoma Mhandisi Elias Mutapima amesema kusaini mikataba hiyo ni kuhakikisha barabara zinapitika katika nyakati zote.
Mhandisi Mutapima amezitaja shughuli watakazokuwa wakitekeleza vikundi hivyo katika matengenezo ya barabara ni pamoja na usafi na kuzibua mitaro, ufyekaji wa nyasi kando kando ya barabara pamoja na kuondoa mchanga barabarani..
Mmoja wa wanachama wa vikundi hivyo, Bw. Haji Said amesema TARURA imetoa fursa ya ajira kwa jamii na kuongeza kwamba vikundi vipo tayari kuhakikisha barabara na mazingira yanakuwa safi na salama wakati wote.

