
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Lucia Renatus (kushoto), akitoa elimu kwa vitendo kuhusu matumizi ya majiko ya umeme yanayotumia nishati safi ya kupikia kwa wakazi wa Mbagala Rangi Tatu, katika Viwanja vya Mbagala Zakhem, Dar es Salaam, Oktoba 8, 2026


Mhandisi Mkuu wa TANESCO Mkoa wa Temeke, David Mhando, (kulia) akiwa na Mhandisi Elirehema Makacha wakitoa elimu kwa vitendo kwa Wananchi kuhusu matumizi ya majiko ya umeme yanayotumia nishati safi ya kupikia.

……….
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limetoa elimu ya matumizi ya majiko ya umeme ya nishati safi ya kupikia kwa zaidi ya wakazi 150 wa Mbagala Rangi Tatu, wakiwemo Mama Ntilie, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia nishati hiyo na kuacha nishati chafu ambazo zinamadhara kwa afya na mazingira.
Akizungumza leo, Oktoba 8, 2026, katika Viwanja vya Mbagala Zakhem, Dar es Salaam, wakati wa zoezi hilo, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Lucia Renatus, amesema matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia yana faida mbalimbali, ikiwemo kuokoa muda wa maandalizi ya chakula kutokana na uwezo wa vifaa vya kisasa vya umeme kuchemsha na kuiva chakula kwa muda mfupi.
Renatus amesema matumizi ya majiko ya umeme husaidia kupunguza moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa ndani ya maeneo ya kupikia, huku akieleza
TANESCO imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya umeme kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi na salama ya vifaa vya kupikia, pamoja na namna ya kutumia umeme kwa ufanisi ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Kwa upande wake, Mhandisi Mkuu wa TANESCO Mkoa wa Temeke, David Mhando, amewasisitiza wananchi kuzingatia kanuni za usalama wanapotumia umeme majumbani na katika maeneo ya kazi, akiwataka kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha ajali na madhara kwa maisha na mali.
Baadhi ya wakazi walioshiriki zoezi hilo wameishukuru TANESCO kwa elimu waliyoipata, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu huduma za shirika, matumizi salama ya umeme na njia sahihi za kuwasiliana na taasisi hiyo wanapohitaji huduma, kutoa taarifa au kupata msaada wa dharura.
Katika zoezi hilo, majiko 10 ya umeme yalinunuliwa na wakazi waliohudhuria, yakiwemo majiko saba ya aina ya pressure cooker na matatu ya induction. Mauzo hayo yamewapa washiriki fursa ya kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ya kupikia katika shughuli zao za kila siku.
Wananchi walipata elimu kuhusu huduma za kidijitali za TANESCO, ikiwemo LUKU Janja na NIKONEKT JISOTI, zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuboresha uzoefu wa wateja.
Elimu hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, yenye kaulimbiu isemayo “Mbele Zaidi Kihuduma.” Kupitia maadhimisho hayo, TANESCO inalenga kuimarisha uhusiano na wateja, kusikiliza mahitaji yao na kutoa elimu inayochangia matumizi bora, salama na yenye tija ya umeme katika jamii.
