BUKOBA, KAGERA – Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Ramadhani Kido, amesema hali ya usalama mkoani humo ni shwari kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea alfajiri ya leo, Oktoba 9, 2026, majira ya saa 11:24 alfajiri.
Taarifa za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa zimeripoti kuwa tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa kati ya 5.0 na 5.2 katika kipimo cha Richter. Hata hivyo, mamlaka za mkoa zinaendelea kufuatilia hali ili kubaini iwapo kuna madhara yoyote yaliyosababishwa na tukio hilo.
Kanali Kido amesema Kitengo cha Maafa mkoani Kagera kinaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo kwa kushirikiana na mamlaka husika, hatua inayolenga kuhakikisha usalama wa wananchi na kupata taarifa sahihi kuhusu athari zinazoweza kuwa zimejitokeza.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na vyombo vya usalama pamoja na wataalamu. Pia, amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini madhara yoyote yanayohusiana na tetemeko hilo.
Wananchi wanashauriwa kufuatilia taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka zinazohusika ili kupata maelekezo sahihi kuhusu hali ya usalama kufuatia tukio hilo la tetemeko la ardhi.
