Na Silivia Amandius – Kagera
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kagera limehitimisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kufanya hafla maalumu iliyowakutanisha wafanyakazi na wateja wao, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika kuadhimisha wiki hiyo, TANESCO Kagera ilianza kwa kutoa elimu kupitia vituo vya redio kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo, pamoja na kutoa tahadhari kwa wananchi kuhusu mvua za El Niño. Baadaye, wafanyakazi na wateja walikutana katika hafla iliyofanyika nje ya ofisi za TANESCO Mkoa wa Kagera, ambapo walishiriki chakula cha mchana, kunywa pamoja na kukata keki katika kuadhimisha wiki hiyo.
Sambamba na hilo, wafanyakazi waliofanya vizuri katika kuwahudumia wateja walitambuliwa na kupewa zawadi kama motisha ya kuendelea kuboresha utendaji wao. Wateja nao walikabidhiwa zawadi ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wao na kuonesha umuhimu wao kwa shirika hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Mhandisi Tumaini Nyari, aliwapongeza wafanyakazi kwa juhudi zao katika kuwahudumia wateja na kuwasisitiza kuendeleza utamaduni wa kutoa huduma bora, zenye ufanisi na zinazokidhi mahitaji ya wateja kila siku.

