Na Silivia Amandius, Bukoba.
Timu 52 za mpira wa miguu na timu 4 za netbool katika Jimbo la Bukoba Mjini zimepokea jezi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Eng. Johnston Mutasingwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza michezo na kuibua vipaji vya vijana katika jimbo hilo. Ugawaji huo umefanyika leo Oktoba 3, 2026 katika viwanja vya Kaitaba, wakati wa bonanza la michezo lililoandaliwa na mbunge huyo.
Akizungumza katika bonanza hilo, Katibu wa CCM Bukoba Mjini, Shabani Mdoe, amewataka vijana kuzitumia jezi hizo kama chachu ya kufikia ndoto zao kupitia michezo, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi na madiwani kuendelea kushirikiana na vijana. Aidha, amesema hali ya baadhi ya viwanja si nzuri na kumtaka Mkuu wa Wilaya kufanya utaratibu kupitia Halmashauri ili viwanja vya michezo vilivyopo katika shule vifanyiwe ukarabati.
Kwa upande wake, Mbunge Johnston Mutasingwa amesema vijana wanapaswa kuchangamkia michezo na kujifunza kutoka kwa wachezaji waliowahi kufanya vizuri. Amesema licha ya yeye kutoa jezi, wadau wengine wa michezo wanaweza kujitokeza kusaidia mahitaji mengine kama viatu na vifaa vya michezo, pamoja na kuwezesha ligi mbalimbali.
Mutasingwa amesema jezi hizo zimetolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya vilabu na si kwa mashindano maalumu, huku akieleza kuwa tayari jozi 52 za jezi zimeshagawiwa. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuibua na kukuza vipaji vya vijana wa Bukoba badala ya kutegemea kuchukua wachezaji kutoka nje ya mkoa.
Aidha, amevitaka vilabu kujisajili ili vitambulike rasmi na ameahidi kusaidia kulipia ada za usajili kwa vilabu hivyo. Amesema utaratibu huo utasaidia kupata wachezaji wenye vipaji ambao wanaweza kufikia kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Championship.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Sima, amepongeza juhudi za mbunge huyo katika kuhamasisha michezo na kusema ataendelea kushirikiana naye katika kuwafikia vijana. Amesema idadi ya vijana wanaopenda michezo ni kubwa na kwamba ugawaji wa vifaa hivyo unaweza kuwa motisha kwao kuendelea kukuza vipaji vyao.
Bonanza hilo limewakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Bukoba Mjini, huku taarifa zikitolewa kuwa Kata zote 14 za jimbo hilo tayari zimepata jezi.

