Na WMJJWM- Dodoma
Viongozi na wawakilishi wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa wameeleza kufurahishwa na ujenzi wa miundombinu inayowezesha kutoa huduma mbalimbali jijini Dodoma.
Wazee hao wameeeleza hayo Oktoba 2, 2026 baada ya kufanya ziara iliyoratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, kwa lengo la kuwezesha wazee hao kujifunza mambo mbalimbali kuhusu miundombinu na vivutio vinavyopatikana jijini Dodoma.
Ziara hiyo ni sehemu ya kuadhimisha siku ya Wazee Duniani ambayo hufanyika Oktoba Mosi kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Novemba 4, mkoani Songwe.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Baraza hilo David Sendo amesema Serikali inaendelea kufanya mambo makubwa katika ujenzi wa miundombinu, jambo linalorahisiha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Tunampongeza Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika ujenzi wa miundombinu, tumejionea kituo cha treni ya kisasa cha Samia Jijini Dodoma ni kizuri sana na tunafurahishwa na hilo, sisi kama wazee tunatoa wito kwa jamii kuendelea kutunza na kutumia vizuri miundombinu hii kwa maslahi ya Taifa”amesema Mzee Sendo.
Baadhi ya maeneo mengine ambayo wazee hao wamtembelea ni Uwanja wa Ndege, Chuo Kikuu cha Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba na Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma.

