Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) iko katika majadiliano na kampuni ya uchimbaji madini ya BuckreeF (BGC) ya Katoro, Geita kwa lengo kukuza ushirikiano wenye nia ya kuandaa nguvukazi mahiri kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kampuni hiyo ya madini, tarehe 1 Oktoba 2026, Meneja wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle amesema miongoni mwa matarajia ya ushirikiano huo ni kupata fursa za mafunzo ya vitendo kwa wakufunzi na wanafunzi wa VETA katika kampuni na kuwajengea uwezo wafanyakazi wake.
“Tumezungumza na uongozi wa Buckreef kuona ni kwa namna gani tunaweza kushirikiana kwanza kwa kuleta wanafunzi wetu wanaosoma fani mabalimbali katika vyuo vyetu ili waweze kupata mafunzo kazini, mafunzo haya yatawawezesha kukomaza ujuzi wao katika stadi wanazojifunza,” amesema Mbelle.
Sambamba na hilo Mbelle amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia mara kwa mara wameomba nafasi za mafunzo kwa ajili ya wakufunzi ili waweze kupata mafunzo zaidi na kuwezesha kutoa mafunzo kulingana na uhitaji wa sasa wa soko la ajira.
Aidha Mbelle amesema kuwa watashirikiana na Buckreef katika kuhakikisaha wananchi wanaozunguka maeneo ya mgodi huo wanapata mafunzo ya ufundi stadi ambapo kampuni hiyo itafadhili mafunzo hayo.
“Buckreef wameona sisi VETA tunaweza kutoa ujuzi kwa vijana wa maeneo haya na sisi tumeona jinsi gani tutaandaa programu za kuweza kuwasiadia vijana wanaozunguka eneo la mgodi kupata ujuzi katika stadi mbalimbali,” amefafanua.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa mgodi huo, Isaac Bisansaba, amewataka wananchi wanaoshi maeneo ya kuzunguka mgodi huo kujiandaa kunufaika na fursa zitakazotokana na ushirikiano wao na VETA.
“Tayari tumekwishaanza mchakato wa kuwatambua vijana waliomaliza kidato cha sita, kidato cha nne au hata wale ambao hawakufaulu kwa viwango vya juu kujiunga nasi, hivyo kuwasaidia kujiunga katika vyuo vya VETA na kulipia sehemu ya mfunzo yao na baadaye kuwapatia nafasi za kufanya mafunzo kwa vitendo katika mgodi wetu,” amesema Bisansaba.

