Na.Sophia Kingimali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Benki ya CRDB kuhakikisha mpango wa kuwawezesha wananchi 500,000 kupata huduma ya umeme unatekelezwa kwa haraka na kuleta matokeo yanayoonekana katika maisha yao.

Ndejembi alitoa agizo hilo leo Octoba 2,2026 wakati wa akizindua wa ushirikiano kati ya Tanesco na CRDB unaolenga kurahisisha na kuwezesha wananchi kupata huduma ya umeme, akisisitiza kuwa uzinduzi huo haupaswi kuishia katika hafla, bali wananchi waanze kuona manufaa yake mara moja.

Alisema ushirikiano huo ni mfano wa namna taasisi za Serikali na sekta binafsi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali katika kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja, hususan katika maeneo ambayo gharama za awali za kuunganishiwa umeme zimekuwa kikwazo.

Ameongeza kuwa, mpango huo unalenga kutoa unafuu kwa wananchi, wakiwamo wanaoishi katika maeneo yenye mazingira yanayofanana na vijiji lakini kutokana na mipaka ya kiutawala wanatambulika kuwa wako mijini na hivyo kukosa baadhi ya unafuu unaopatikana kwa wananchi wa vijijini.

Amesema katika mpango huo, CRDB itawezesha wananchi katika maeneo yaliyolengwa kupata ruzuku ya gharama za kuunganishiwa umeme, huku kwa maeneo mengine wananchi watakapewa fursa ya kulipia gharama hizo kidogo kidogo kupitia mfumo wa ufadhili wa benki.

Ndejembi amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa umeme ni msingi wa maendeleo ya jamii, akieleza kuwa huduma hiyo inahitajika na wanafunzi kwa ajili ya kusoma, wakulima kuongeza thamani ya mazao, vijana kutumia teknolojia na wabunifu kuendeleza kazi zao, pamoja na wafanyabiashara kuongeza tija katika shughuli zao.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo kwa kukosa huduma muhimu.

Ndejembi alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa umeme, akibainisha kuwa vijiji 12,318 vilivyosajiliwa Tanzania Bara vimefikiwa na huduma hiyo, huku kazi ikiendelea kuwaunganisha wananchi waliopo katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa kikamilifu.

Amesema maendeleo hayo yanaendana na utekelezaji wa mipango ya Taifa, ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo, pamoja na malengo ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati ili kuchochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji, ajira na ubunifu.

Akizungumzia hali ya Dar es Salaam, Ndejembi amesema ukuaji wa idadi ya watu, viwanda na shughuli za kiuchumi umeongeza mahitaji ya umeme, jambo lililofanya Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu mipya ya umeme ili kuongeza uwezo wa jiji hilo kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Naye Waziri wa Nishati, Juma Homera, aliipongeza Tanesco na CRDB kwa kuanzisha ushirikiano huo, akisema ni hatua muhimu katika kuongeza kasi ya kuwafikishia wananchi huduma ya umeme na kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuongeza kiwango cha upatikanaji wa nishati nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo imeamua kutumia uwezo wake wa kifedha, teknolojia na mtandao wake kusaidia kuondoa vikwazo vinavyowakabili wananchi katika kupata umeme, akisisitiza kuwa taasisi hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika miradi ya maendeleo.

Naye,Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema ushirikiano kati ya shirika hilo na Benki ya CRDB utaongeza kasi ya kuwaunganisha wananchi wanaokosa huduma ya umeme kutokana na kushindwa kumudu gharama za kuunganishiwa kwani amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hiyo muhimu.

Twange ameongeza kuwa TANESCO ina jukumu la kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme, na kwa sasa nchi ina umeme wa kutosha pamoja na miundombinu inayozidi kupanuliwa. Hata hivyo, amesema changamoto iliyobaki ni baadhi ya wananchi ambao miundombinu imefika katika maeneo yao lakini hawana uwezo wa kugharamia maunganisho, hali inayochelewesha kufikiwa kwa lengo la kuongeza idadi ya wateja wa umeme.

Amesema kupitia mpango huo, TANESCO itashirikiana na CRDB na viongozi wa serikali za mitaa kuwawezesha wananchi wanaostahili kupata huduma hiyo bila kubebeshwa mzigo wa gharama za awali, huku mpango huo ukianza kwa majaribio katika maeneo yatakayokubaliwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliomba Serikali kuendelea kuipa kipaumbele mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kutokana na ongezeko kubwa la watu, shughuli za viwanda na mahitaji ya umeme, akisema uwekezaji katika nishati ni muhimu kwa kuendeleza uchumi na kuongeza fursa kwa wananchi.