Na Mwandishi wetu, Geita
WAZIRI wa Madini Anthony Peter Mavunde amesema sekta ya madini hadi Juni 30,2026 imeingiza Sh 1.393 trioni kwenye mfuko wa Serikali huku asilimia 40 ikitokana na wachimbaji wadogo.
Waziri wa Mavunde ameeleza hayo kwenye siku ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini katika maonyesho ya tisa ya kimadini ya teknolojia ya madini yanayofanyika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan, Manispaa ya Geita.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wizara hiyo ililenga kukusanya Sh 351 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka ambapo hadi sasa imekusanya Sh 411bilioni hivyo kuonyesha namna sekta hiyo inavyozidi kukua.
Amesema kila mwaka migodi mikubwa iliyopo nchini hutumia Sh 5.1trioni kwa mwaka katika manunuzi ya bidhaa na huduma ambapo Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 90 ya Sh5.1 trilioni zinazotumika kila mwaka kununua bidhaa na huduma katika sekta ya madini zinabaki nchini.
“Fursa hizo zinatarajiwa kuongezeka kutokana na kampuni 14 zinazotarajiwa kuanzisha miradi mikubwa ya madini pamoja na leseni 28 za uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) ambazo Serikali imekuwa ikizitaka zianze uzalishaji,” amesema.
Waziri Mavunde amesema kampuni hizo zimetoa ajira 19,000 huku asilimia 96 wakiwa ni wazawa ambapo wizara hiyo imelenga kuifanya sekta ya madini kuongoza katika utoaji wa ajira nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti amempongeza Waziri Mavunde kwa namna anavyoongoza Wizara hiyo kwa uchapakazi na uadilifu.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Dkt Janet Lekashingo amesema ushirikishwaji wazawa kwenye kampuni za madini halipaswi kuishiwa kwenye ajira pekee na badala yake kampuni za kizawa zijielekeze kwenye zabuni zinazotolewa kupitia ushindani ili kunufaisha jamii za wazawa kwenye sekta ya madini.
Mbunge wa Geita Mjini Chacha Wambura amemuomba Waziri Mavunde kufuatilia utekelezaji wa sheria hiyo ya ushirikishwaji wazawa (local contrent) kufuatilia baadhi ya kampuni za kigeni ambazo kwasasa zimegeuka kuwa za kizawa bila uwepo wa uwazi wa mabadiliko hayo.
“Pamoja na kufanya hili jambo nikuombe uendelee kufuatilia kwa nguvu zote ili uwaone hata wale wanaojaribu kudanganya,unaweza ukakuta leo kampuni A ilikuwa ya kigeni lakini kesho unaikuta ni ya kizawa,wakati mwingine unashindwa kujua mbona hatukuona wakiuza hisa?”
