NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amekabidhi mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Sadani, Kata ya Nzihi, Wilaya ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya awali ya kuchangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi huo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kiswaga alisema alikumbushwa ahadi hiyo aliyotoa wakati wa mkutano alioufanya katika eneo hilo mwezi Agosti, ambapo aliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji ili kusaidia wananchi kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo.
Kiswaga alisema awali alitarajia kutoa mifuko yote 50, lakini kutokana na mahitaji mengine yaliyopo katika jimbo hilo, ameamua kuanza na mifuko 20 huku akiahidi kumalizia mifuko iliyobaki na kushirikiana na wananchi hadi ujenzi wa ofisi hiyo utakapokamilika.
“Nilifanya mkutano hapa mwezi wa nane na wenzangu walinikumbusha kwamba niliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji ili waweze kujenga ofisi ya kijiji. Leo nimeleta mifuko 20 na tutaendelea kushirikiana hadi tutakapomaliza,” alisema Kiswaga.
Alisema maendeleo yanahitaji ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na Serikali, akieleza kuwa pamoja na Serikali kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali, bado kuna changamoto katika maeneo ya elimu, afya na miundombinu ambazo zinahitaji nguvu za pamoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sadani, Davis Msela, alimshukuru Mbunge Kiswaga kwa kutimiza sehemu ya ahadi yake na kuunga mkono juhudi za wananchi katika ujenzi wa ofisi hiyo.
Msela alisema Kiswaga aliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo, na kwamba makabidhiano ya mifuko 20 yameongeza nguvu katika kuendeleza mradi huo, huku mifuko 30 ikiwa bado inahitajika ili kutimiza ahadi hiyo.
Alisema ujenzi wa ofisi hiyo ni muhimu kutokana na hali ya jengo la zamani ambalo limechakaa na kuwa na changamoto katika kipindi cha mvua, hali inayowalazimu wananchi na viongozi kufanya vikao katika mazingira yasiyo salama hivyo tunahitaji kukamilisha ofisi hii haraka ili tuweze kuhamia kwenye ofisi mpya,
Alisema thamani ya ujenzi wa jengo hilo inakadiriwa kufikia Sh milioni 47, huku hadi sasa wananchi na wadau mbalimbali wakiwa wameendelea kuchangia na tayari takribani Sh milioni mbili zikiwa zimetumika katika hatua za awali za ujenzi.
Aidha, aliipongeza kazi inayofanywa na Mbunge Kiswaga katika Jimbo la Kalenga, akisema amekuwa akitoa msaada katika maeneo mbalimbali, yakiwemo shule, zahanati na ofisi za vijiji.
Alisema wananchi wa Sadani wana matumaini kuwa kwa kuendelea kushirikiana na viongozi wao, watafanikiwa kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo na kuanza kuitumia kwa shughuli za kijiji.
Alisema wananchi wanaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na viongozi wao katika kutatua changamoto za maendeleo, akisisitiza kuwa miradi ya kijamii inahitaji ushiriki wa pamoja ili iweze kukamilika kwa wakati.

