Na Farida Mangube Morogoro 

Mkwawa Group of Campaign imekabidhi kisima chenye thamani ya Shilingi milioni 38 kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika eneo la Makunganya, Morogoro.

Kisima hicho kitatumika katika shughuli za uhifadhi, ikiwemo kuotesha na kulea miche ya miti, huku pia kikiwanufaisha wakazi wa maeneo ya jirani ambao awali walilazimika kutembea hadi kilomita 10 kutafuta maji safi na salama.

Akizungumz Katika hafla ya Kukabidhi kisima hicho Mkurugenzi wa uzalishaji kiwanda Cha Mkwawa David Mayunga amesema wameamua kuunga mkono shughuli za uhifadhi zinazotekelezwa na TFS, huku akiwataka wananchi kukitunza kisima hicho ili kiendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Morogoro na Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti Mohamed Msalu amesema kisima hicho kimefika wakati muafaka kutokana na mkakati wa TFS wa kuongeza uzalishaji wa mbegu na miche ya miti.

Amesema pia kisima hicho kitapunguza changamoto ya maji kwa jamii inayozunguka shamba hilo na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na wahifadhi.

Msalu ameishukuru Mkwawa Group of Campaign kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi na utalii ikolojia, akisema miundombinu hiyo pia itasaidia shughuli mbalimbali za uhifadhi ndani ya shamba.

Nae Recho Mapenza mkazi wa Makunganya, ameishukuru TFS na Mkwawa Group of Campaign, akisema kisima hicho kimewapa unafuu wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji.

Amesema wananchi wataendelea kushirikiana na TFS katika kutunza kisima hicho na kulinda mazingira yanayowazunguka.