TUME ya Ushindani (FCC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) imetoa mafunzo kwa wafanyabishara na wajasiriamali wa Wilaya ya Geita ambao wanashiriki katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini ili waweze kukuza biashara zao.
Mafunzo hayo ambayo yametolewa leo Oktoba 1, 2026 ni sehemu ya Kliniki ya Biashara iliyo chini ya Mwamvuli wa TanTrade ambapo Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwemo FCC zinashiriki kutoa huduma kwa wananchi katika Maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Akizungumza na wajasiriamali katika Banda la Wilaya ya Geita, Bw. Nsajigwa Wilfred, Afisa Uhusiano wa Umma Mkuu FCC, amesema lengo kubwa la kushiriki katika Maonesho hayo ni kutoa huduma kwa wafanyabishara na wajasiriamali ili waweze kufahamu majukumu ya msingi ya Tume hiyo hususan katika kulinda na kushajiisha ushindani wa biashara, kudhibiti bidhaa bandia, kumlinda mlaji ikiwa ni pamoja na kupokea maoni au ushauri wa kitaalam kuhusu changamoto zinazowakabili na kuona namna bora ya kuzitafutia majawabu muafaka kwa wakati sahihi.
Aidha, Bw. Nsajigwa amebainisha kuwa FCC ina jukumu la msingi katika kusimamia na kutekeleza Sheria ya Ushindani Namba 8 ya Mwaka 2003 (FCA) ambayo ina jukumu la kulinda na kushajiisha ushindani wa biashara ili kuhakikisha ushindani wa biashara unafanyika kwa haki na kwa kuzingatia misingi madhubuti ya sheria, kanuni na taratibu katika nyanja ya uchumi wa soko.
”Jukumu lingine ni kumlinda mlaji yaani mtumiaji wa mwisho wa huduma na bidhaa, pia tuna jukumu la kusimamia Sheria ya Alama za Bidhaa kwa kuhakikisha kwamba hakuna bidhaa yoyote inayozalishwa, kusambazwa au kuuzwa ambayo ni bandia, ” amesema Nsajigwa.
Afisa huyo wa FCC amewashauri wafanyabiashara na wajasiriamali kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa na alama zilizosajiliwa ili kuhakikisha usalama wa bidhaa na kumlinda mlaji.
Bw. Nsajigwa ametoa rai kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kuitumia fursa ya Kiliniki ya Biashara inayopatikana katika Maonesho hayo ili kupata huduma na utatuzi wa changamoto mbalimbali za kibiashara na katika sekta ya ushindani kwa ujumla.
Kwa upande wake Bw. Deo Shayo, Meneja Ukuzaji Biashara wa TanTrade, amewaasa wafanyabiashara na wajasiriamali hao kusajili bidhaa zao kwa chapa ya ‘Made in Tanzania’ ili ziweze kutambulika kimataifa na kuipa nguvu chapa ya Tanzania ili kuimarisha uchumi na kuchochea uwekezaji na uzalishaji.
”Mjisikie fahari kuuza bidhaa zenu zikiwa na chapa ya Made in Tanzania ili kuipa nguvu chapa ya Tanzania, kuimarisha uchumi na kuchochea uwekezaji na uzalishaji, ” amesema Shayo.

FCC, TANTRADE ZATOA MAFUNZO KWA WAFANYABIASHARA GEITA
