Na Hellen Mtereko,

Mwanza

Wananchi wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza wanatarajiwa kunufaika na kambi maalumu ya matibabu itakayohusisha madaktari bingwa na bingwa bobezi kutoka ndani na nje ya nchi kwaajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa,kutoa elimu na matibabu.

Hayo yamebainishwa jana na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, John Nzilanyingi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofsini kwake.Amesema kambi hiyo itahusisha magonjwa ya moyo,mapafu na mishipa ya damu,uchunguzi wa dalili za awali za saratani,kisukari na shinikizo la damu pamoja na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Alisema katika Kambi hiyo huduma zote zitatolewa bure hivyo aliwasisitiza wananchi kuanza kujiandikisha kwenye zahanati zilizoko kwenye maeneo Yao kwaajili ya kushiriki kikamilifu .

Alisema kambi hiyo itafanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na itaanza kuanzia Oktoba 9 hadi 12 mwaka huu, ambapo wananchi watapata huduma za uchunguzi na matibabu, ikiwemo operesheni ndogo na kubwa.

Alisema madaktari watakaotoa huduma wanatoka katika taasisi mbalimbali za afya, zikiwemo Taasisi ya Kansa ya Jakaya Kikwete(JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI na Ocean Road, pamoja na madaktari kutoka nchini India,Pamoja na madaktari kutoka hospitali ya Rufaa ya Bugando, Hospital ya Nyamagana na Sekoutoure.

“Madaktari hawa watakuja kwajili ya kutibu wananchi magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo hivyo nawaomba wenye changamoto za kiafya katika sehemu mbalimbali kuweza kujisajili katika maeneo yao ili tuweze kupata idadi yao” alisema.

Katika hatua nyingine, Kwa upande wa huduma ya maji, Nzilanyingi amesema changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Nyamagana inaendelea kushughulikiwa kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo mradi wa maji wa Butimba.

Alisema zaidi ya Sh bilioni 76 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji, huku akiishukuru Serikali kwa hatua hizo na kumuomba Waziri wa Maji, Juma Aweso kusaidia kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika.

Kuhusu miundombinu ya barabara, Mbunge huyo lisema wananchi wamekuwa wakilalamikia uharibifu wa baadhi ya barabara na kuitaka Serikali kuhakikisha ubora wa kazi katika ujenzi na matengenezo ya barabara unasimamiwa ipasavyo.