Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini India, imewapokea jumla ya mawakala wa utalii 13 kutoka India kwa ajili ya ziara maalum ya utangazaji utalii (Familiarization Trip) itakayofanyika nchini kuanzia tarehe 28 Septemba 2026 hadi 04 Oktoba, 2026.
Lengo kuu la ziara hii ni kuwapa fursa mawakala hao kujionea vivutio vya utalii vilivyopo nchini, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati yao na wadau wa utalii wa Tanzania.
Akizungumza kuwakaribisha nchini Mawakala hao, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega ambaye ameongozana na ujumbe huo, amesema Ubalozi utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii kutoka India katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kukuza sekta hiyo na kuchangia Uchumi wa nchi na kwamba ziara ya mawakala hao ni moja ya jitihada za Ubalozi huo katika kuhakikisha vivutio vya utalii vinatangazwa nchini India kupitia mawakala hao.
Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Mawakala hao ambaye pia ni Rais na Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha shughuli za Utalii cha India, Bw. Himanshu Patil amesema kuwa lengo la ziara yao hapa nchini ni kujionea vivutio vya utalii na kuzungumza na wadau muhimu katika sekta hiyo ili hatimaye kuwawezesha kushirikiana na Tanzania katika kuwafikia watalii kutoka India kuja nchini.
Kabla ya kuanza kwa ziara hiyo, mawakala hao walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo ya kibiashara (B2B) na kundi la waendesha shughuli za utalii (Tour Operators) kutoka Tanzania. Mkutano huo ulilenga kujenga mahusiano ya kibiashara ya moja kwa moja na kufungua fursa mpya za kukuza idadi ya watalii kutoka soko la India.
Ziara hii ni sehemu ya mkakati endelevu wa Bodi ya Utalii Tanzania wa kukuza soko la India ambalo kwa sasa ni miongoni mwa masoko sita yanayoongoza kwa kuleta watalii nchini.
Wakiwa nchini Mawakala hao watatembelea maeneo mbalimbali ya utalii yakiwemo Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Zanzibar.

