Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Afisa Maendeleo Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwelinde Katto, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha hatua za kulinda mtoto kwa kutengeneza na kutekeleza sheria ndogondogo katika ngazi za halmashauri na vijiji.Ameyasema hayo Septemba 30, 2026 jijini Dodoma, wakati wadau kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wataalamu wa Serikali walipokutana Septemba 29 na 30, 2026 kujadili namna ya kuimarisha ulinzi wa haki za mtoto wa kike, hususani katika kukomesha ndoa za utotoni.

Amesema jamii inapaswa kupewa elimu kuhusu mila na desturi zenye madhara kwa watoto, huku viongozi wa dini, wazazi, walezi, watoto na watu mashuhuri wakishirikishwa katika juhudi hizo. Pia amesisitiza kuwa watu wenye ushawishi katika jamii watambuliwe na kupewa uwezo wa kusaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Aidha , amebainisha Kuwa ni muhimu kuwa na mipango ya kuwasaidia watoto ambao tayari wameathirika, wakiwemo kina mama vijana, pamoja na kukabiliana na umaskini kwa kutumia fursa za mikopo, miradi ya TASAF na mifumo mingine iliyopo katika jamii.

Amesema mifumo ya ulinzi wa mtoto inapaswa kuimarishwa kwa kuongeza wataalamu na bajeti, huku teknolojia za kidijitali zikitumika katika kuwafuatilia watoto walio katika hatari, kuripoti changamoto na kuchukua hatua mapema.

Kwa upande wake, Afisa Daraja la II kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Evelyne Soi, amesema kuna haja ya kuoanisha sera na sheria zinazohusu watoto na vijana ili kuondoa mkanganyiko katika utambuzi na ulinzi wa haki zao.

Amebainisha Kuwa Sera ya Maendeleo ya Vijana inamtambua kijana kuwa mwenye umri wa miaka 15 hadi 35, wakati sheria ya mtoto inamtambua mtoto kuwa mtu mwenye umri chini ya miaka 18, hivyo kundi la wenye miaka 15 hadi 17 linajikuta likitambuliwa kwa namna tofauti katika nyaraka hizo.

Amesema elimu ya ulinzi wa mtoto inapaswa kuanzia katika ngazi ya familia ili jamii itambue madhara ya ndoa na mimba za utotoni pamoja na aina nyingine za unyanyasaji, huku akitaka rasilimali watu na fedha ziongezwe katika taasisi zinazotekeleza sera hizo.

Aidha, amependekeza mapitio ya sheria mbalimbali, ikiwemo zinazohusu mirathi na ardhi, ili kuimarisha ulinzi wa watoto na kuhakikisha masuala yao yanazingatiwa bila kujali jinsia.

Wadau hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kuimarisha ulinzi wa haki za mtoto, ikiwemo kuongeza elimu kwa jamii, kuboresha mifumo ya ulinzi na kuoanisha sera na sheria zinazohusu watoto ili kukabiliana na changamoto za ndoa za utotoni na aina nyingine za ukatili dhidi ya watoto.