Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) akiagana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Palamagamba Kabudi mara baada ya kumaliza ziara yake wilayani Kilosa, Septemba 29, 2026. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akiwa kwenye ziara wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, Septemba 29, 2026. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Palamagamba Kabudi na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akielezea jambo wakati wa ziara yake Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Septemba 29, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akikagua Daraja la Magufuli Mto Kilombero alipokuwa kwenye ziara wilayani humo, Septemba 29, 2026. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Dustan Kyobya
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Dustan Kyobya akimwelezea jambo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wakati akikagua Daraja la Magufuli Mto Kilombero alipokuwa kwenye ziara wilayani humo, Septemba 29, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Palamagamba Kabudi alipokuwa kwenye ziara yake wilayani Kilosa, Septemba 29, 2026. Kulia ni Mhandisi Lusajo Edwin – Afisa Kidakio cha Wami kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu.
………….
NA MWANDISHI WETU
IFAKARA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ametoa siku saba kwa Bodi ya Maji Bonde la Mto Rufiji kukamilisha ujenzi wa tuta katika Mto Lumemo, eneo ambalo maji yake yamekuwa yakisababisha athari kwa wananchi wa Kata ya Ipangalala, Wilaya ya Kilombero.
Masauni ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake wilayani Kilombero mkoani Morogoro Septemba 29, 2026, iliyolenga kukagua hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na athari za mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha.
Amesema kuchelewa kukamilisha ujenzi wa tuta hilo kunaweza kuongeza madhara kwa wananchi, hasa kutokana na utabiri wa mvua kubwa katika maeneo mbalimbali.
“Maisha ya binadamu ni muhimu sana kuliko fedha ambazo tutatumia kujenga eneo hili. Hivyo, natoa wiki moja wahusika wawe wamekamilisha ujenzi kwa kuwa muda uliopo si rafiki kutokana na utabiri uliotolewa kuhusu mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha,” amesema Masauni.
Aidha, Waziri Masauni amewataka wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na kuepuka utupaji wa taka ovyo, akisema baadhi ya taka husababisha kuziba kwa mifereji ya maji na kulazimisha maji kuhama njia, jambo linaloweza kusababisha uharibifu wa miundombinu na mali za wananchi.
“Nipende kusisitiza kila mmoja wetu kuhakikisha tunatunza mazingira yetu kwa kupanda miti, kutotupa taka hovyo ambazo mwisho wa siku zinaziba mifereji na kusababisha maji kuhama njia na kuleta uharibifu kwenye miundombinu,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wa mvua hizo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kupata elimu kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mafuriko na majanga yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Afisa wa Maji Bonde la Kilombero, Abisai Chilunda amesema tuta hilo lina urefu wa takribani kilomita 11, huku akieleza kuwa kazi zitakazo fanyika kwa haraka ni katika maeneo yaliyoathirika na mvua zilizonyesha.
“Tutakamilisha ujenzi huo kwa wakati kama ambavyo Waziri ametuelekeza ili kukimbizana na muda kwa kuweka mawe katika maeneo yanayotakiwa na kujaza udongo katika maeneo mengine ambayo yalikuwa yamepasuka,” amesema Chilunda.
Amesema Bonde la Kilombero limekuwa likishirikiana na wananchi katika kudhibiti maeneo yenye changamoto kwa kujenga matuta na mifereji, hatua inayolenga kurahisisha mtiririko wa maji na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa.
Naye Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Elibariki Bajuta amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabonde kuhama na kwenda maeneo salama, huku akisisitiza umuhimu wa kuacha ukataji miti ovyo.
Bajuta pia amewataka wananchi kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki, akisema taka hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuziba mitaro na mifereji ya kupitisha maji, hali ambayo inaweza kuongeza ukubwa wa athari wakati wa mvua kubwa.
Katika ziara hiyo, Masauni na ujumbe wake walikagua maeneo mbalimbali yenye changamoto za kimazingira na miundombinu, likiwemo eneo la ujenzi wa tuta la Reli ya SGR kuanzia Mkundi hadi Lukobe, Mto Diwale katika Kata ya Kichangani, Turiani, eneo la Dumila katika Mto Kikundi, Mto Mkondoa–Kidete katika Kata ya Kasiki, pamoja na Mto Lumemo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
