Na Ashrack Miraji | Same, Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapande, amewataka wananchi na watumishi wa umma kutumia mvua zinazotarajiwa kunyesha kutokana na hali ya El Niño kupanda miti kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Mapande ametoa wito huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Amesema pamoja na tahadhari zinazotolewa kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, wananchi wanapaswa pia kuzitazama kama fursa ya kupanda miti, kwani unyevu wa mvua utasaidia miche kustawi vizuri.
Amesema upandaji wa miti kwa wingi utasaidia kulinda mazingira, ikiwamo kupunguza mmomonyoko wa udongo, huku akiwataka wananchi kuanza zoezi hilo mapema kabla na wakati wa mvua.
“Pamoja na tahadhari tunazotoa kuhusu mvua hizi, tutumie pia fursa hii kupanda miti kwa wingi. Miti ikipata mvua kwa wakati itastawi vizuri na baadaye itasaidia katika kulinda mazingira na kupunguza mmomonyoko wa udongo,” amesema.
Aidha, amewataka madiwani kwenda kutoa elimu katika kata zao na mashuleni kuhusu umuhimu wa upandaji miti, akisisitiza kuwa wananchi wapande miti ya kawaida pamoja na miti ya matunda.
Amesema hatua hiyo itaunga mkono kampeni ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Kaslida Mgeni, ya kuifanya Same kuwa wilaya ya kijani, hivyo amewataka wananchi kuanza utekelezaji wake mapema.
Katika hatua nyingine, Mapande amemtaka Mkuu wa Idara ya Kilimo kuanzisha hamasa ya kilimo cha mazao ya kimkakati, hususan zao la parachichi, ili wananchi wanufaike na fursa hiyo.
Amesema baada ya kipindi cha El Niño, idara hiyo inapaswa kuandaa taarifa itakayoonyesha idadi ya miche ya parachichi iliyopandwa pamoja na kata ambazo zimefanikiwa katika kilimo hicho.
“Baada ya miaka mitatu tunahitaji kujua tumefikia wapi. Tuwe na kumbukumbu ya idadi ya miparachichi iliyopandwa, kata gani imefanya vizuri na ni matokeo gani tunayotarajia baada ya mvua hizi,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Same Mamndolwa Gembe amesema wananchi hawapaswi kuzitazama mvua hizo kwa upande wa madhara pekee, bali wazitumie pia kama fursa ya kupanda miche ya mazao mbalimbali ambayo inaweza kuwasaidia kiuchumi baadaye.
Amesema mvua hizo pia zinaweza kutumika kama fursa ya kuvuna na kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi ya kilimo cha umwagiliaji, badala ya kuyaacha maji yapotee bila kunufaisha jamii.

